Na Mwandishi wetu.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kutafuta fedha za kuwalipa fidia wananchi waliopitiwa na Miradi ya kufua umeme ya Ruhudji na Rumakali, ili wananchi hao wapishe maeneo hayo na waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku wakati miradi hiyo ikisubiri kutekelezwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Same Mhe. David Mathayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika Mkoa wa Njombe, tarehe 16 Machi 2025.
Mhe. Mathayo amesema, Serikali itafute fedha za kuwalipa fidia wananchi walioathiriwa na miradi hiyo ili wananchi hao wapishe na meneo hayo na waendelee na shughuli zao zingine wakati serikali ikiendelea kutafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo.
“ Tayari tathmini imeshafanyika kwa wananchi watakaopitiwa na mradi huo na gharama za kuwalipa zimefahamika,na wananchi wanayo hiyo taarifa, ni vyema sasa serikali ikatafuta fedha za kuwalipa fidia wananchi hao ili wakaendelee na Maisha yao mengine wakati juhudi za kutekeleza mradi hiyo zikiendelea kufanyika”, alisisitiza Mhe. Mathayo.
Utekelezaji wa Miradi ya Ruhudji na Rumakali utaiwezesha nchi kupata zaid ya megawati 500 za umeme ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuimarisha hali ya upatikanai wa umeme nchini.
Kamati hiyo imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupelekea umeme kwa wananchi wake kama alivyoahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kusema kuwa ni jambo la msingi sana kwa kuwa wananchi wamekuwa wakisubiri umeme huo kwa muda mrefu na kwa miaka mingi .
Alifafanua kuwa kuna maeneo mengine ni magumu kufikika kwa kuwa hakuna miundombinu ya Barabara na ambayo wananchi wake walikuwa hawajawahi kupata huduma ya umeme tangu enzi za uhuru, lakini kwa sasa wamepata umeme kutokana na umakini wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwajali wananchi wake.
#NTTupdates