×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

BOTI HII ITUMIKE KWA KUZINGATIA MWONGOZO ULIOPO-DKT. YONAZI

Na Mwandishi wetu.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kukabialiana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu, usafirishaji wa dawa za kulevya, biashara za magendo na utoroshwaji wa nyara za serikali katika Bahari na Maziwa yote nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 19, 2024 na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati wa hafla ya makabidhiano ya Boti ya Doria (PB SAILFISH) iliyofanyika katika Chuo cha Bahari (DMI) Jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt. Yonazi amesema, lengo kuu la kununuliwa kwa boti hiyo ni kuimarisha doria ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu nchini, hivyo, boti hiyo itatimiza lengo na kuimarisha juhudi za Serikali za kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika eneo lote la bahari.

“Ni matumaini ya serikali kuona boti hii inatumika ipasavyo katika shughuli zilizopangwa na zitakazojitokeza kwa mujibu wa mahitaji ya matumizi kwa wakati husika.

Aidha, naomba kuwasisitizia kuwa matumizi ya boti hii pia yazingatie Mwongozo wa Kitaifa wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu wa mwaka 2022”, alisema Dkt. Yonazi.

Aidha, Dkt. Yonazi amewataka wadau na mashirika kuendelea kufanya kazi na Idara ya Menejimenti ya Maafa iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuweza kuratibu programu za uokozi kwa majanga ya majini na usalama wa bahari kwa ujumla na kuwashukuru wafadhili kwa ufadhili na ushirikiano walioutoa wakati wa ununuzi wa boti hiyo.

“Ninaomba kutumia nafasi hii kuwajulisha kuwa, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ina imani kubwa na uwezo wa TASAC katika usimamizi, uendeshaji na utunzaji wa boti hii, hiyo ndiyo sababu iliyopelekea boti hii kukabidhiwa kwa shirika hili.

Ni imani yetu kuwa mtaitunza vizuri ikiwa ni pamoja na kuifanyia matengenezo kinga kwa wakati na hivyo kuwaongezea ufanisi katika kazi zenu za kila siku hususani katika ukaguzi kwa meli zinazoingia kwenye maji yetu ya ndani” alisema Dkt. Yonazi.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Bw. Ludovick Nduhiye amesema, boti hiyo itakuwa ni jibu katika utekelezaji wa malengo na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola pamoja na wadau wa sekta ndogo ya usafirishaji majini katika kudhibiti wa vitendo vya kiuhalifu katika maeneo ya mwambao wa bahari na Maziwa Makuu.

“Kukabidhiwa kwa boti hii kwa Shirika letu la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imekuwa chachu katika kutimiza kwa vitendo Dira yetu ambayo imelenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye huduma za uchukuzi na hali ya hewa yenye uhakika, usalama na nafuu” alisema Bw. Nduhiye.

#NTTupdates