×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

CHANGAMKIENI FURSA ZA UJIO WA MADAKTARI BINGWA-DKT KAGYA

Na Mwandishi wetu.

WANANCHI Mkoani Lindi, wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujio wa madaktari bingwa bobezi wa Rais Samia, watakaotoa huduma za kibingwa katika hospitali za Wilaya zote,huduma itakayo punguza adha ya kwenda umbali mrefu kufuata huduma hizo kwa gharama kubwa.

Rai hiyo, imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dkt. Kheri Kagya, leo Septemba 16, 2024 wakati wa kuwapokea madaktari hao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo watakaotoa huduma kwa muda wa siku Sita.

“Tunayo furaha kuwapokea madaktari Bingwa na wahudumu wengine wa Afya ambao mtakwenda kuhudumia Hospitali za Halmashauri Sita za mkoa wa lindi, katika kipindi hicho cha siku Sita mtatoa huduma kwa wananchi mbao yumkini wasingeweza kusafiri kuja Hospitali ya mkoa kupata huduma hizo ama kwenda Hospitali ya Kanda au ya Taifa, hivyo natoa rai kwa wananchi wote kutumia fursa hii adhimu kupata huduma hizi bobezi na za Kibingwa huko Wilayani.” Amesema Dkt. Kagya.

Aidha, Dkt. Kagya amesema madaktari hao watakuwepo kwa muda wa siku Sita kuanzia leo Septemba 16 hadi 21 wakitoa huduma hizo za kibingwa kwenye Hospitalli zote za Halmashauri mkoani Lindi na huduma hizo zitatumia bima na kwa wagonjwa wasio na bima watamuona daktari kwa kuchangia kiasi kidogo kwa utaratibu wa kawaida kama atahitajika kupata huduma nyingine ikiwemo vipimo, upasuaji au dawa.

“Gharama za kumuona daktari kwenye kambi hii ya siku Sita mkoani hapa haitakuwepo, hivyo wananchi watakao kuja kumuona daktari bingwa watamuona bure pasipo kulipia ila watachangia huduma nyingine zitakazo hitajika baada ya hapo.” Amesema Dkt. Kagya

Dkt. Kagya ametaja aina ya madaktari waliowapokea ni pamoja na madaktari bingwa wa huduma za magonjwa ya kike na uzazi, upasuaji, mfumo wa mkojo, magonjwa ya ndani, huduma za mifupa, watoto, ganzi pamoja na usingizi.

Awali, akizungumzia lengo la kufanya huduma hizo za kibingwa mwakilishi kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni mratibu wa madaktari hao waliotoka hospitali mbalimbali nchini Tanzania Bi. Faraja Mgeni amewakumbusha Madaktari hao kwenda kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kuzingatia maadili ili kutimiza lengo la Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Afya kwa wananchi huku akiomba waganga wakuu kwenye Halmashauri kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kutimiza majukumu yao.

“Niaombe viongozi wetu, waganga wa kuu wa Hospitali hizo za Halimashauri kuwapa ushirikiano madaktari bingwa pamoja na wauguzi na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupata huduma hizi kwani zinawapunguzia gharama.” Amesema Bi. Faraja

#NTTUpdates