Na Mwandishi wetu.
MKUU wa Wilaya ya Dodoma Jabiri Shekimweri amesema Ofisi za Taifa za Takwimu barani afrika zinatakiwa kuendelea kuzalisha Takwimu rasmi na zenye ubora na kuzisambaza kwa njia rafiki na za kuaminika kwa wakati ili kuwezesha Serikali na wadau kufanya maamuzi yanayohusu utekelezaji wa eneo huru la biashara barani afrika.
Shekimweri ameyasema hayo leo Novemba 20 jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika ambapo amesema kuwa wakati Ofisi hizo zikifanya hayo hazina budi kuboresha mifumo ya ushirikiano wa kitakwimu ili Takwimu ziweze kuwafikia wadau kwa urahisi na kwa usahihi kwa kuzingatia matumizi ya njia rahisi za usambazaji wa Takwimu husika.
“Kwa kushirikiana na Ofisi za Takwimu za afrika zitakuwa zinatekeleza lengo namba 17 la malengo endelevu ya Dunia ambalo linahimiza ushirikiano katika kutekeleza malengo hayo ambayo Nchi za afrika zimeridhia utekelezaji wake,”amesema Shekimweri.
Aidha amesema kuwa Ofisi za Taifa za Takwimu barani afrika zinawajibu mkubwa wa kusaidia Nchi kufanya maamuzi yanayohusu sera kuhusiana na eneo huru la biashara Afrika.
Shekimweri amesema Takwimu zinakuwa na maana pale ambapo zinatolewa taarifa kwani zinakwenda kukidhi mahitaji kwa usahihi na idadi husika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa shughuli za kitakwimu NBS Emilian Karugendo amesema kuwa matumizi ya Takwimu rasmi ndio msingi wa kila kitu katika maisha,katika mipango na katika kufuatilia programu mbalimbali na utekelezaji wake.
#NttUpdates