×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

DKT. BITEKO AITAKA BODI YA TANESCO KUENDELEZA VYANZO MSETO VYA UMEME

Na Mwandishi wetu.

SERIKALI imesema kuwa nishati ya umeme ni nguzo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi ya Taifa na kuwa inachochea shughuli za uzalishaji viwandani, huduma na kuboresha maisha ya wananchi.

Na ni matarajio ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona umeme wa uhakika unafika kwa kila Mtanzania ili kuimarisha maendeleo na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko Septemba 15, 2024 jijini Dar es salaam wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

‘’ Namshukuru na kumpongeza Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri na ufuatiliaji wake wa karibu wa utendaji kazi wa wizara na taasisi za Serikali ili ziweze kutimiza vyema majukumu yake.

Tunafurahi kuwa Bodi hii iliteuliwa wakati muhimu sana kwa TANESCO. Kwani mradi mkubwa wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) tayari umeanza kuzalisha umeme na megawati 705 tayari zimeingizwa kwenye Gridi ya Taifa,”Ameendelea

“ Ni jukumu la Bodi kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa wakati ili Taifa letu liweze kufurahia matunda yake,’’ amesema Dkt. Biteko.Amesisitiza

‘’ Ni muhimu kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati, ikiwemo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, mfano mradi wa Malagarasi mkoani Kigoma na miradi mingine ya uzalishaji iliyopo katika hatua za utekelezaji.

Pia, kuhakikisha tunaendeleza vyema vyanzo mseto vya umeme ikiwemo mathalani mradi wa umeme wa jua Kishapu mkoani Shinyanga na uendelezaji wa nishati ya jotoardhi nchini.’

’Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza Bodi hiyo mpya ya TANESCO kwa kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika na kuitaka kuongeza jitihada za kuimarisha huduma kwa wateja huku akiwataka kutojihusisha na vitendo vya udalali katika zabuni zitakazotangazwa na Shirika.‘’

Nataka niwahakikishie kuwa Serikali na Watanzania wanataka wapate umeme wa uhakika na walipe kama walivyotumia na sio kulipa kwa gharama kuliko walivyotumia, wanataka nishati safi ya kupikia hivyo mhamasishe pia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Sisi Wizarani tumejiwekea kipimo cha kupimana kila robo mwaka tunakutana na kuangalia utekelezaji wa kila taasisi na nyie Bodi sasa wapimeni watu wenu.’’ Amemaliza Dkt. Biteko.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba amesema ‘’ Tangu kuwepo kwa Bodi hii mpya malalamiko kuhusu TANESCO yamekuwa yakipungua na hii ni ishara kuwa Bodi imekuwa ikisimamia vizuri Shirika.’’ Amesema Mhandisi Mramba.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho amesema kuwa Bodi imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka Wizarani sambamba na kupata wajumbe wa Bodi wenye sifa, vigezo na utaalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.

Aidha, Dkt. Nyansaho amesema wameendelea kushirikiana na Wizara kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ya upatikanaji wa umeme ambayo kwa sasa imepungua na hivyo wamejikita katika usambazaji wa umeme.

Akizungumzia kuhusu kuwezeshwa kwa wakandarasi wa wazawa ili waweze kushiriki katika miradi ya TANESCO Dkt. Nyansaho amesema ‘’Ni vizuri katika manunuzi wakandarasi wazawa wapewe uzito kwa sababu inaweza kuwa asilimia kubwa ya fedha inaenda nje ya nchi, hii haimaanishi tusiwape wageni zabuni kubwa ila baadhi ya sehemu tuwape watu wa ndani na wakiwezeshwa wanaweza kusaidia kuchachua uchumi wa nchi yetu.’’

#NTTupdates