×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

DKT. BITEKO ASISITIZA UMUHIMU WA ELIMU USALAMA MAHALA PA KAZI

Na Mwandishi wetu.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko mewataka waajiri kwa kushirikiana na wadau wanaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza usalama mahala pa kazi na kuwawezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira rafiki na hivyo kukuza uzalishaji na kupunguza gharama za uzalishaji.

Dkt. Biteko amesema hayo (leo Aprili 28, 2024) Jijini Arusha katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa kazi Duniani.

” Niwatake waajiri na waajiriwa kuhakikisha usalama mahali pa kazi, mtu wa kwanza kujali usamala wake ni mwajiriwa, ukiona mtambo hauko salama toa taarifa kwa mwajiri wako; hapa hautaonekana umegoma bali ni kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama “, amesema Dkt. Biteko.

Ameitaka OSHA kwa kushirikiana na wadau katika masuala ya usalama mahali pa kazi kuhakikisha wafanyakazik wanakuwa na mazingira yatakayowawezesha kuwa salama na kupata furaha na matumaiani kisha kupata ari ya kuendelea kufanya kazi na kuongeza ufanisi kazini.

Amehimiza OSHA kuendelea kutoa elimu kuhusu wa usalama mahali pa kazi badala ya mfumo wa kizamani ambapo mwajiri na mwajiriwa walikuwa wakiogopana na kuhofiana kutokana na kufanya kazi za “KIPOLISI” Amesema pamoja na hatua zinazochukuliwa kutoa elimu, bado elimu zaidi inahitajika kuhakikisha kwamba pande husika zinaendana na matakwa ya kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobasi Katambi akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali inashirikiana ILO kuhakikisha Tanzania inazingatia usalama na afya mahala pa kazi.

” Serikali ina wajibu wa kilinda nguvu kazi ya Taifa kwa kuwa afya njema ni mtaji wa nguvu kazi pia tunasheria ya kuhakikisha afya ya mzalishaji inalindwa”, amesema. Katambi.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri (ATE) ametoa wito kwa Serikali na Waajiri kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa inayozingatia usalama na afya mahala pa kazi.

Aidha, Mwakikishi wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bi. Juliana Mpanduji amesema kuwa TUCTA itaendelea kushirikiana na Serikali, OSHA na ATE ili kulinda nguvu kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Madhimisho hayo ya Siku ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi yenye kauli mbiu “Athari za Mabadiliko ya Nchi katika Usalama na Afya Kazini: Jisajili na OSHA kushiriki Mapambano dhidi ya Athari hizo” yameambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi.

#NTTUpdates