×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

ILEMELA YAJA NA MIKAKATI YA KUONDOA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI

Na Mwandishi wetu, Mwanza.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza, imedhamiria kuondoa vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na uzazi kwa kuweka huduma za kisasa za upasuaji na wodi za akina mama na watoto kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya Wilayani humo.

Hayo yamebainishwa leo katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alipotembelea na kukagua ujenzi wa wodi ya kisasa ya mama na mtoto kwenye Zahanati ya Nyakato inayojengwa kwa Tshs. Milioni 227 ,ambapo hadi sasa imefikia asilimia 85 ya utekelezaji huku ikitumia fedha kutoka mapato ya ndani.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, amewapongeza Viongozi na Watendaji wa Wilaya hiyo kwa usimamizi mzuri ambao unaonesha dhamira njema ya kuhakikisha akina mama wanajifungua salama na kuondoa kabisa vifo vya uzazi Wilayani humo.

Mtanda amewataka Halmashauri hiyo kukamilisha ndoto na nia yao nzuri kwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na kwa ubora ili akina mama wasipate tena msongamano kwenye Hospitali za Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure na Kanda Bugando.

Katika hatua nyingine Mtanda amekagua kiwanda cha vijana cha kufyatua matofali (Vision Community team work) kilichopo kwenye mtaa wa Kahama na akawapongeza vijana hao kwa kukopa na kurejesha Tshs. Milioni 40 kutoka Halmashauri na kukuza mtaji hadi milioni 60.

#NTTUpdates