×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

JAMII YATAKIWA KUACHA DHANA POTOFU UONGOZI WA WANAWAKE

Na Mwandishi wetu.

Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid, ameitaka jamii kuachana na dhana potofu kwamba wanaume pekee ndio wenye uwezo wa kuwa viongozi bora kuliko wanawake.

Dkt. Maulid ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam, katika Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililoandaliwa na Programu ya Shule Bora kwa kushirikiana na ADEM, likijadili nafasi ya wanawake katika uongozi wa sekta ya elimu ambalo limehudhuriwa na Walimu, Maafisa Elimu wa Mikoa, Wilaya na Kata, Viongozi wa Wizara ya Elimu, Viongozi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Watendaji wa Vyuo Vikuu, Wanafunzi wa Elimu ya Juu, pamoja na wadau wa elimu kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema “Jamii inapaswa kubadili mtazamo wa kizamani unaodhani kuwa wanaume pekee ndio wenye uwezo wa uongozi. Tunahitaji kumwangalia mwanamke kwa mtazamo chanya, tukitambua uwezo wake wa kuleta mabadiliko katika uongozi.”

Ameongeza kuwa mitazamo hasi dhidi ya wanawake ndio sababu iliyopelekea Programu ya Shule Bora na ADEM kuandaa kongamano hilo ili kujadili changamoto zinazowakwamisha wanawake kushika nyadhifa za uongozi katika sekta ya elimu, pamoja na kuibua mikakati madhubuti ya kuwawezesha.

Kwa upande wake, Bi. Aziza Ally, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamakonge – Kibiti, amesema kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa uongozi na wanapaswa kupewa nafasi za kuchangia maendeleo ya taifa na kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo kuwa mwanamke anaweza kuwa kiongozi bora licha ya changamoto za mtazamo hasi wa jamii.

Naye Bi. Indo Palla, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kaunda – Rufiji, amebainisha kuwa wanawake ni waadilifu na wachapakazi, hivyo wakipewa fursa za uongozi watachangia maendeleo ya taifa kwa ufanisi mkubwa

#NTTUpdates