×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

MADARASA MAPYA YAPUNGUZA MSONGAMANO NGUDU SEKONDARI

Na Mwandishi wetu.

Wananchi Wilayani Kwimba wameishukuru Serikali, kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya madarasa 10 na ofisi 4 za walimu katika shule ya sekondari Ngudu ambapo wamesema miundombinu hiyo imesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.

Hayo yamejiri leo tarehe 11 Oktoba, 2024 wakati mwenge wa uhuru ulipofanya ufunguzi wa miundombinu hiyo chini ya kiongozi ndugu Godfrey Mnzava.

Akiongea baada ya ufunguzi huo, kiongozi huyo amesema Rais samia ameamua kuboresha miundombinu ya elimu nchini ili kuwa na kizazi bora cha sasa na baadaye na akatoa rai kwa wanafunzi kutunza miundombinu hiyo ili iweze kuwasaidia wao na wanafunzi wenzao siku zijazo.

Naye Mkuu wa shule hiyo Mwl. Wilbard Mchele amesema mahitaji ya miundombinu ni madarasa 31 na iliyopo ni 25 na kwamba kumekua na ongezeko kubwa la wanafunzi lililopelekea msongamano darasani hivyo ujenzi wa madarasa hayo umeondoa msongamano darasani

“Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, tunaishukuru serikali kwa kutuletea fedha hizi ambazo pamoja na kupunguza msongamano utasaidia pia kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia pamoja na kuongeza ufaulu wa wanafunzi kutokana na kuboresha mazingira.” Mwalimu Mchele.Amefafanua.

Halikadhalika, ndugu Mnzava amefungua mradi wa maji katika kijiji cha Mhulya uliotekelezwa kupitia fedha za serikali kuu (PforR) wenye uwezo wa kuzalisha lita 12,336 kwa gharama ya shilingi milioni 667.1 ambao utawanufaisha wananchi 3,147 wa kijiji hicho.

#NTTUpdates