×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

MAKALLA AZINDUA MSIMU WA TOHARA KWA JAMII YA KIMASAI

Na Mwandishi wetu.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, Oktoba 20, 2025, amezindua sherehe za msimu wa tohara kwa jamii ya Kimaasai nchini Tanzania, akiishukuru jamii hiyo kwa kuheshimu sheria na miongozo ya nchi kwa kusimamisha shughuli za tohara Oktoba 29, 2025 ili kuruhusu makundi rika mbalimbali kwenda kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo.

Sherehe hizo maarufu kama Enkipaata zimezinduliwa kwenye Kijiji cha Oldonyosapu, Wilaya ya Arumeru, zikitarajiwa kuhusisha zaidi ya vijana 2,000 wa kundi rika la Irmegoliki litakalodumu katika hadhi hiyo mpaka Oktoba 2032, akiwahakikishia usalama na amani wakati wote kuanzia sasa, siku ya upigaji wa kura na baada ya upigaji kura.

Makalla pia amewahimiza wananchi wote kushiriki kuchagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi huo.

“Ninawashukuru kwanza kwa kunipa heshima ya kuzindua sherehe hizi, na zaidi ni kwamba pamoja na kuwa na mila zenu bado mmeheshimu taratibu na ratiba nyingine za serikali.

Niwaombe tarehe 29 viongozi wote mpaze sauti katika maeneo yote, watu wapate haki ya kupiga kura, na sisi kama serikali tuwahakikishie kuwa uchaguzi utakuwa salama na wenye amani,” amesema Makalla.

Kwa upande wake, kiongozi mkuu wa jamii ya Kimasai, Isack Meijo Ole Kisongo, na mlezi wa kundi rika hilo linaloingia kwenye msimu wa tohara, amesema wataiheshimu Oktoba 29, 2025 kwa kuwa jamii hiyo inatambua umuhimu wa upigaji wa kura.

#NTTupdates.