Na Mwandishi wetu.
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema hakuna maendeleo endelevu na ya haraka endapo Wanawake hawatashirikishwa na kuwezeshwa Ipasavyo Kiuchumi.
Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation amesema hayo alipozungumza na timu ya Watendaji wa Shirika la Action Aid Tanzania Waliofika Ofisini kwake Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa bado kuna Kazi kubwa ya kufanya inayohitaji Ushirikiano wa Taasisi hizo mbili Ili kuwainua Wanawake Kiuchumi Hususani Wakulima wa zao la Mwani.
Ameainisha eneo jengine la Ushirikiano kuwa ni Mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wa Jinsia wanavyofanyiwa Wanawake na Watoto alilosema linahitaji kuwa na Mkakati Maalum wa kuwajengea Uwezo wa kupaza sauti zao na kutambua haki zao za Msingi.
Mama Mariam Mwinyi amefahamisha kuwa tatizo la muhali ni kubwa linaloikabili Zanzibar Katika Juhudi za kukabiliana na Vitendo vya Udhalilishaji.
“Ninatamani kuona Watoto wote wanafundishwa kujua haki zao ili kuwalinda na Udhalilishaji” alisisitiza Mama Mariam.
Akizungumzia Mradi wa Maji Safi na Salama kwa Wanafunzi uliowasilishwa na Action Aid katika Kikao Kazi hicho amesema ni Mradi Muhimu utakaowahakikishia Wanafunzi Upatikanaji wa maji Salama wakiwa Skuli pamoja na kuwalinda na Magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji Yasio salama.
Ameihakikishia Action Aid Tanzania kuwa Zanzibar Maisha Bora Foundation iko tayari kushirikiana nao kufanya Kazi kwa Ukaribu zaidi kuyafikia Matarajio na Malengo ya Taasisi hizo ambayo yanafanana.
#NTTUpdates