Na Mwandishi wetu.
Mke wa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Gueta Selemane Chapo, ametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) za jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Mama Gueta amepongeza ubora wa huduma za kibingwa na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utoaji wa matibabu.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mama Gueta Chapo amepokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi, na kufafanuliwa kuhusu huduma zinazotolewa katika vitengo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kitengo cha Tiba ya Uzazi kwa Njia ya Kisasa (IVF), wodi ya kina mama waliojifungua, na huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima zinazotolewa JKCI.
Aidha, akiwa katika wodi ya wanawake waliojifungua, Mheshimiwa Mama Chapo amepata fursa ya kukutana na akina mama waliolazwa, ambapo alitoa zawadi na kusisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa mama na mtoto, akitaja kuwa huo ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.
Katika Kitengo cha IVF, Mheshimiwa Mama Chapo ameelezwa kwa kina kuhusu huduma zinazotolewa kwa wanawake na wanaume wenye changamoto za uzazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mama Chapo ameonesha kuvutiwa na mafanikio ya huduma hiyo na kubainisha umuhimu wa kuimarisha huduma kama hizo nchini Msumbiji.Vilevile, akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Mheshimiwa Mama Chapo amepata maelezo kuhusu huduma za kibingwa za upasuaji na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima.
Pia ameshuhudia kazi ya madaktari bingwa na kupongeza ubora wa huduma zinazotolewa, pamoja na mchango wa ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha huduma hizo.
Katika mazungumzo yake na viongozi wa hospitali hizo, Mheshimiwa Mama Chapo ameeleza kufurahishwa na kiwango cha huduma na teknolojia inayotumika katika MNH na JKCI, huku akisisitiza kuwa uzoefu alioupata utasaidia kuanzisha ushirikiano wa kina kati ya Msumbiji na Tanzania, hususan katika maeneo ya afya ya moyo, huduma za uzazi na matibabu ya kibingwa.
#NTTUpdates