Na Mwandishi wetu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bwana Balandya Elikana, leo tarehe 10 julai, 2025 katika ukumbi wa Gold Crest jijini Mwanza amefungua Mkutano wa wadau wa Kilimo, Uvuvi na wajasiriamali chini ya mradi wa Kijani Space kwa ushirikiano na Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO).
Akizungumza na wajumbe wa Mkutano huo ambao ni watafiti na wakulima Bw. Balandya, amewataka kwenda kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji walio ngazi ya chini na kufanya shughuli zao kwa Kilimo kinachozingatia tahadhari ya uharibu wa mazingira ili kujihakikishia uendelevu.
Amesema kuwa, wananchi wa ukanda wa ziwa victoria ni kielelezo cha shughuli za kila siku za watanzania kwani jamii inajihusisha na uvuvi na kilimo kama shughuli rasmi zinazowajenga uchumi wao hivyo mradi wa Kijani Space ni tunu kwa makundi hayo endapo malengo yatazingatiwa.
“Kilimo kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kinachangia zaidi ya asilimia 70 na uvuvi kwa zaidi ya asillimia 10 kwenye pato la taifa hivyo sisi kama Mkoa tutashirikiana na wadau wa mradi huu kuboresha shughuli za wananchi zinazowaingizia kipato kila uchwao.” Amesema Bw. Balandya.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri shughuli za uchumi kama ukame na uchafuzi wa mazingira kutokana na kushuka kwa uzalishaji hivyo basi kwa kuwafikia makundi hayo ni jambo jema kwa faida ya jamii nzima kwani watapata uelewa wa namna ya kuhifadhi mazingira.
Vilevile, amewakaribisha wadau hao kutalii kwenye vivutio vya utalii kama Kisiwa cha Saanane na kufanya utalii wa ziwa Victoria ili waweze kuona urithi wa Tanzania na kuweza kupumzika ndani ya mkoa huo wenye hali ya hewa nzuri na usalama.
Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mwanza Bw. Bakari Songwe amesema lengo la jukwaa hilo ni kutambulisha mradi ambao unajumuisha wadau wanaohusika kutoka ukanda wa Afrika Mashariki mathalani watanzania ili kuungana na wajumbe kutoka Kenya na Uganda.
#NTTupdates