×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

RAIS SAMIA AHIMIZA KASI UKUAJI SEKTA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA

Na Mwandishi wetu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameibadilisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili wizara hiyo ijikite katika kukuza sekta ya mawasiliano na teknolojia ndani na nje ya nchi.

Ameyasema hayo leo Desemba 10, 2024 Ikulu ndogo Tunguu, Zanzibar wakati akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni.Amefafanua kuwa, ilipokuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, sekta ya habari ilipewa msukumo mkubwa, hivyo ameitoa sekta hiyo ili wizara hiyo ijikite kwenye teknolojia ya habari pamoja na mawasiliano ndani ya nchi na kuiunganisha Tanzania na nchi zingine kupitia Mkongo.

Pia, isimamie Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Shirika la Posta yasimame na kuwa mashirika ya kibiashara.

“Kwa kuwa tunakwenda na kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano na teknolojia dunia nzima na tuna mkakati wa uchumi wa kidijitali wa kitaifa ambao ni mkubwa na unatakiwa kushughulikiwa peke yake, nimeunda Wizara hii mpya ili ijikite katika shughuli hizo.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa maagizo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi kuisimamia sekta ya habari kwani anafahamu vyema masuala ya habari. Pia kumpa msukumo Naibu Waziri, Mhe. Hamis Mwinjuma kusimamia sekta zilizosalia.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kuwa viongozi walioapishwa wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu yale ambayo Watanzania wanayahitaji.

“Tunawasihi kufanya kazi ambayo Mhe. Rais Samia na Watanzania wanatarajia muifanye, mkashirikiane na viongozi ambao mtawakuta katika nafasi zenu, mkaheshimu mawazo ya wataalam ambao mtawakuta katika vituo vyenu vya kazi”, amesema Dkt. Mpango.

Vile vile, ametoa rai kwa Mabalozi walioapishwa kuifanya vyema ajenda ya kidiplomasia ya kiuchumi ili jitihada ya Rais Samia kupitia falsafa ya R4 iweze kutekelezwa kwa ukamilifu.

#NTTupdates