Na Mwandishi wetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda, kufuatia kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali (Mstaafu) David Bugozi Musuguri.
Kupitia ukurasa wa Instagram Rais Samia ametoa pole Kwa Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi pamoja na Makamanda, wapiganaji wastaafu, wapiganaji walio katika utumishi, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa kuondokewa na shujaa huyo.
“Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda, Makamanda, wapiganaji wastaafu, wapiganaji walio katika utumishi, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa kuondokewa na shujaa wetu, mpendwa wetu, mwalimu, mshauri na kiongozi wetu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali (Mstaafu) David Bugozi Musuguri.
”Amesema Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha yake ya miaka 104, ambapo miaka 46 kati ya hiyo ameitumikia nchi kwa weledi, umahiri, kujituma, ushujaa, nidhamu na kwa mafanikio ya hali ya juu, akiishi kiapo chake cha kuwa tayari kuutoa uhai wake ajili ya ulinzi wa Taifa letu.
Ametuachia mfano bora wa utumishi wa umma utakaoendelea kuwa mwanga ndani na nje ya Majeshi yetu.Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali David Musuguri, amefariki Dunia leo, Oktoba 29, 2024, jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu.
Jenerali Musuguri, aliyezaliwa Januari 4, 1920 huko Butiama Mkoani Mara, aliitumikia Nchi katika Jeshi kuanzia Mwaka 1942 hadi 1988, akihitimisha Uongozi wake kama Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kati ya 1980 na 1988.
Alianza kazi yake kijeshi katika King’s African Rifles (KR) na Tanganyika Rifles kabla ya kujiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Jenerali Musuguri aliongoza majeshi ya Tanzania katika vita dhidi ya Idi Amin Dada wa Uganda Mwaka 1978, baada ya uvamizi wa eneo la Kyaka, Mkoani Kagera.
Mapambano na vita alivyoshiriki ni pamoja na Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Battle of Madagascar, Vita vya Kagera, na Battle of Simba Hills.
#NTTUpdates