×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

RC MTANDA ATOA SIKU 14 WAFANYABIASHARA WALIOSHINDA ZABUNI SOKO KUU LA MJINI KATI KUHAMIA

Na Mwandishi wetu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amekagua shughuli za biashara katika soko kuu jipya la mjini kati jijini Mwanza na kuagiza ndani ya siku 14 wafanyabiashara zaidi ya 100 walioshinda zabuni na kugawiwa maeneo kuanza mara moja biashara.

Ametoa agizo hilo baada ya ukaguzi aliobaini uwepo wa vizimba na maeneo ya wazi 109 ambayo tayari yameshapata wafanyabiashara kupitia mchakato wa zabuni uliofanywa katika mfumo wa TAUSI bila sababu za msingi.

Mhe. Mtanda amesema Serikali imejenga soko hilo kwa zaidi ya Bilioni 26.6 lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya soko la awali ambalo lilikua finyu na kupelekea wafanyabiashara 807 kuhamishiwa katika Soko la Mbugani kwa muda.

Aidha, amewataka wote wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi kuondoka mara moja na kurudi kwenye masoko rasmi ili kuweka unadhifu ndani ya jiji hilo na kuwa na taswira iliyopangwa.

“Hatuwezi kukaa kimya tukaacha miji yetu inachafuliwa, hatua kali zichukuliwe kwa wote wanaoziba barabara kwani tusipokua na utaratibu na kazi zetu hatuwezi kupanga mambo yetu.”

Akizungumzia wafanyabiashara waliokosa vibanda na vizimba sokoni hapo, Mhe. Mtanda amesema Mwanza ina watu zaidi ya milioni 3.6 na walioko jiji pekee ni zaidi ya milioni 1 hivyo sio rahisi kukidhi maeneo 1464 na ndio maana kuna mpango wa kujenga masoko mengine hivyo wawe na subira.

Akimuwakilisha Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Afisa biashara wa jiji hilo Bi. Madelina Mtweve amebainisha kuwa 2018/19 wafanyabiashara 807 walihamishwa kutoka kwenye soko hilo na 2019/20 ukaanza ujenzi wa soko jipya la kisasa.

“Mhe. Mkuu wa Mkoa, baada ya uboreshaji hivi sasa soko lina maduka 522, vizimba, mabucha, meza 504, vyoo 3 vyenye matundu yanayotesheleza mahitaji, stoo 15, migahawa midogo 12, machinjio 167 na eneo la kuegesha magari 159.” Bi. Mtweve.

#NTTupdates