Na Mwandishi wetu.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 20 hadi 50 kwenye mitungi ya gesi ya LPG takribani 452,445 kwa watumiaji wa mwisho ikiwa ni jjtihada za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 23, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Grace Tendega aliyetaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa muda mfupi wa kuhakikisha Wananchi wa Vijijini wanatumia Nishati Safi ya kupikia badala ya Kuni na Mkaa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti Serikali kupitia REA pia itasambaza majiko banifu 200,000 yenye bei ya punguzo la hadi asilimia 75 pamoja na kuwezesha ufungaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma zinazohudumia watu zaidi ya 100.” Amesema Kapinga
Aidha, amesema Serikali imekamilisha kazi ya usambazaji umeme katika vijiji vyote hivyo kwa sasa inaendelea kuhimiza matumizi ya majiko ya kupikia yanayotumia umeme ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa vijijini badala ya kutumia kuni na mkaa.
Mhe. Kapinga ametanabaisha kuwa, Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ni wa miaka kumi lakini Serikali inao mkakati wa matumizi bora ya nishati ambao unahusisha pia sekta binafsi kwa ajili ya kusaidia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akijibu swali la Mbunge wa Mbulu, Mhe. Zacharia Isaay aliyeuliza Serikali imejipangaje kuhakikisha Vitongoji vyote vilivyokusudiwa katika mwaka huu wa bajeti kufikiwa na umeme katika kipindi cha mwezi mmoja uliobaki, Mhe. Kapinga amesema Serikali inayo mikakati na miradi mbalimbali ya kupeleka umeme katika Vitongoji.
Amesema kuwa, moja ya mikakati hiyo ni kupeleka umeme katika Vitongoji 15 kwa kila Jimbo, na pia Serikali imekuja na mkakati wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo awamu ya kwanza inaanza kupeleka umeme katika Vitongoji 9000 na hatua iliyopo ni utafutajj wa wakandarasi.
#NTTupdates