Na Mwandishi wetu.
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, ametangaza rasmi kuwa kuanzia tarehe 1 Mei 2025, Tume kwa kushirikiana na vyombo vya utekelezaji wa sheria itaanza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya taasisi zote zitakazoshindwa kujisajili kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na. 11 ya mwaka 2022.
Akizungumza jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Dkt. Mkilia amesisitiza kuwa sheria hiyo inazitaka taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya, kuchakata, au kuhifadhi taarifa binafsi kuhakikisha zinasajiliwa na Tume ili kulinda usalama wa taarifa za wananchi.
Kwa kutoa fursa ya mwisho kwa taasisi ambazo bado hazijakamilisha usajili wao, Dkt. Mkilia alieleza kuwa taasisi hizo zina hadi tarehe 30 Aprili 2025 kukamilisha mchakato huo.
Ameonya kuwa taasisi zitakazoshindwa kutimiza wajibu huo zitakumbana na hatua kali za kisheria, ikiwemoKutozwa faini ,Adhabu za kisheria, na Hatua nyingine zilizoainishwa katika Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Hatua hii inafuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Rais alihimiza taasisi zote za umma na binafsi kuwasilisha usajili wao kwa Tume kama sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha ulinzi wa taarifa binafsi kwa mujibu wa sheria.
Dkt. Mkilia amesema kuwa serikali imedhamiria kuimarisha mifumo ya ulinzi wa taarifa binafsi ili kulinda faragha za wananchi na kuongeza uwajibikaji wa taasisi zote nchini.
“Hii ni hatua muhimu katika kufanikisha ajenda ya mabadiliko ya kidijitali nchini. Ulinzi wa taarifa binafsi si tu hitaji la kisheria, bali pia ni kiashiria cha kuimarisha haki za wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 16(1),” amesisitiza.
Dkt. Mkilia ameongeza kuwa uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi utachangia Kuimarisha usalama wa taarifa za kidijitali, Kuwajengea wananchi imani kwa taasisi za umma na binafsi, naKufanikisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
Tume imeelekeza taasisi zote zilizobaki kukamilisha usajili kabla ya muda uliowekwa. “Hatutaacha kuchukua hatua stahiki dhidi ya taasisi zitakazokaidi sheria.
#NTTupdates