×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

SERIKALI KUINGIZA TRILIONI 10 KWA KUUZA MAZAO YA KIMKAKATI NJE YA NCHI.

Na Mwandishi wetu.

NAIBU Waziri wa Kilimo David Silinde ameeleza kwamba Serikali itaingiza kiasi cha fedha dola za marekani 3.5 bilioni kwa mwaka kwa kuuza mazao ya kimkakati nje ya nchi kwa mwaka.

Silinde ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 19, 2024 jijini Dodoma kwenye Uzinduzi wa mchakato wa kufungua masoko mapya ya mazao ya kipaumbele katika nchi mbalimbali.

Amesema hivi sasa nchi imepata kibali cha kuuza mazao tisa ya kiupaumbele kwenye nchi 14 ambayo yataliingizia taifa kiasi cha fedha Dola za Marekani 3.5 bilioni na kuwataka wakulima nchini kuchangamkia fursa hiyo.

Aidha Silinde ameyataja mazao hayo ya kipaumbele kuwa ni nanasi, ndizi, tumbaku, parachichi, viazi mviringo, karafuu, pilipili manga, vanilla, na kakao ambayo yatauzwa kwenye nchi 14 duniani.

“Nchi hizo ni pamoja na China ambao wanahitaji vanila na nanasi, India (vanilla na nanasi), Indonesia (karafuu), Singapore (karafuu), Israeli (parachichi), Malaysia (parachichi), Uturuki (nanasi), Brazili (nanasi), USA (kakao), Afrika kusini (ndizi), Zambia (viazi mviringo), Pakstani (tumbaku) na Iraq (tumbaku).”amesema Silinde.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya kilimo imejipanga kufanya maboresho ili kuondoa vikwazo katika usafirishaji wa mazao ya kilimo yananyohitajika katika mataifa mbalimabali duniani ili kuinua uchumi wa taifa kupitia sekta hii.

Naibu waziri huyo amesema inakadiriwa kuwa uuzaji wa mazao nje ya nchi utaiwezesha serikali kupata jumla ya dola za Marekani 3.5 bilioni ambazo ni sawa Sh10 trilioni za kitanzania ambazo zinaweza kuongezeka kama thamani ya mazao haya itaongezwa.

Mmoja wa wasafirishaji wa mazao nje ya nchi Mohamed Adamjee amesema kufunguliwa kwa masoko ya mazao nje ya nchi yanatoa fursa kwa wakulima na wafanyabiashara kuongeza bidii kwenye shughuli zao za kilimo kwa sababu wana uhakika wa kuuza.

Amesema kitendo cha nchi 14 kufanya biashara ya mazao na Tanzania kinawahakikishia wakulima kufanya biashara kuliko kuwa na nchi chache ambapo yakitokea majanga kama vile vita, magonjwa ya mlipuko au uchumi wa nchi kuyumba kunasababisha biashara kusimama.

#NTTupdates