Na Mwandishi wetu.
Katika jitihada za kuboresha afya ya jamii, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ameongoza kikao na Makamu wa Rais wa Masuala ya Tiba na Sayansi wa Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation la nchini Marekani (EGPAF), Dkt. Anja Giphart, juu ya umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na maambukizi ya UKIMWI kwa watoto, akieleza kuwa hili si tu suala la kiafya bali pia ni jukumu la kijamii linalogusa mustakabali wa vizazi vijavyo.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam leo Disemba 10, 2024 katika ofisi ndogo za Wizara ambacho kimelenga kutathmini mafanikio na changamoto zinazohusu juhudi za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuimarisha huduma za afya kwa watoto na vijana wenye maambukizi.
Aidha, Dkt. Mollel amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau kama EGPAF ili kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa huru dhidi ya UKIMWI, huku akisisitiza kuwa juhudi hizi zinapaswa kwenda sambamba na uwekezaji wa ndani na uendelevu wa miradi ya afya.
Pia Dkt. Mollel amelipongeza shirika la EGPAF, kwakuwa linaongoza duniani katika vita dhidi ya UKIMWI kwa watoto na limechangia kiasi kikubwa nchini Tanzania kupitia miradi kama USAID Afya Yangu Northern na mpango wa RAS+, ambao umesaidia kuboresha huduma za afya, kupunguza maambukizi na kuimarisha mifumo ya afya kwa familia nyingi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Masuala ya Tiba na Sayansi wa Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Dkt. Anja Giphart amesema azma ya shirika hilo ni kuendelea kutoa huduma kwa jamii ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa rasilimali za kutosha na hitaji la kuimarisha huduma za upimaji na matibabu katika kliniki za uzazi.
#NTTUpdates