×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

TATHMINI NI KIOO – RC MTANDA

Na Mwandishi wetu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema kufanya tathmini ni muhimu, inakufanya uone na kutambua nguvu na udhaifu hivyo ameifananisha kama kioo ambapo amesema kinatoa fursa ya kujitazama.

Mkuu wa Mkoa amesema hayo wakati alipokuwa akifungua kikao cha Watumishi wa Sekta ya Ardhi Mkoa wa Mwanza na kuipongeza sekta hiyo kwa wazo hilo kwani watapata fursa ya kutambua na kurekebisha mahali walipokosea ili waweze kufikia malengo.

“Mtu yoyote anayependa maendeleo lazima ajifanyie tathmini ya mwaka mzima, ni watu wachache wanaopenda kufanya tathmini, unapojitathmini utajua wapi pa kurekebisha”

Aidha, Mhe. Mtanda amekitaka kikao hicho kutokujikita katika sekta ya ardhi pekee bali pia kuwafanyia tathmini wale aliowaita wasukumaji wa sekta hiyo ( Wataalamu wa Ardhi).

“Mnaweza kukaa humu ndani mkajifungia mkaongea na mpaka muda wa chakula ukafika mkala lakini kumbe mnafanya tathmini ya uongo, sasa ni lazima muambiane ukweli” Amesema Mkuu wa Mkoa.

Kadhalika Mkuu wa Mkoa amewataka Wataalamu wa Ardhi kushughulikia migogoro ya ardhi kwa kudhibiti kutokuibuka kwa migogoro mipya na kushughulikia migogoro iliyopo kwa weledi.

Kuhusu ukusanyaji wa maduhuli, Mkuu wa Mkoa ameitaka sekta hiyo kuhakikisha wanaongeza hamasa na ufuatiliaji katika ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha elimu ya ulipaji kodi ya ardhi inatolewa mara kwa mara ili kuwepo na ushirikishwaji wa wananchi.

Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo kwa Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha kunakuwepo na operesheni za Wilaya kwa Wilaya kuhusu kliniki za ardhi walau mara mbili kwa mwaka.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza Bw. Wilson Lugi amesema wamekutana kama wataalam kufanya tathmini ya kiutendaji ya mwaka 2024/2025 na kupanga namna ya kufanya vyema 2025/26.

Kamishna huyo wa Ardhi Msaidizi amesema wametekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa hati, usimamizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali, Pia wamefanikiwa kukusanya maduhuli ya Serikali zaidi ya sh. bilioni 8.7 sawa na 42% ya makusudio.

#NTTupdates