×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

TUSIWATENGE WALA KUWANYANYAPAA WATOTO WENYE USONJI – MAJALIWA

Na Mwandishi wetu.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii ya Watanzania kuacha kuwanyanyapaa watoto na watu wanaoishi na Usonji, magonjwa ya mfumo wa fahamu pamoja na matatizo ya akili.

Pia amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye changamoto za ukuaji au uelewa watafute ushauri kwa wataalam wa afya ili watoto wao waweze kufaidika na huduma zilizopo katika umri mdogo.

“Wataalam wetu muendelee kuongeza juhudi katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa haya ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na huduma.” Ametoa wito huo leo ( Jumapili 28, Aprili 2024) alipokuwa akizungumza baada ya kushiriki mbio fupi za hisani za Run 4 Autism Tanzania, zilizofanyika katika viwanja vya The Green Ground Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

Kadhalika ameiagiza Wizara ya Afya kuongeza vituo vya huduma za uchunguzi hasa utambuzi wa mapema wa ugonjwa wa usonji na matatizo mengine ambayo yanaweza kubainika wakati watoto wanapoenda kwenye kliniki kila mwezi.

“Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI zihakikishe uwepo wa huduma jumuishi zinazoweza kuleta tija kwa kina mama na watoto ambao wanazaliwa na magonjwa ambayo yanaweza kubainika mapema”

Aidha, ameitaka Wizara ya Elimu iendelee kongeza kasi ya upanuzi wa utoaji wa huduma za Elimu Jumuishi pamoja na kuongeza wigo wa mafunzo na vyumba vya madarasa katika shule nyingine ili watoto wenye ulemavu wasitembee umbali mrefu kwenda shule.

Naye, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS), imeanzisha Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Mazoezi tiba ya kusaidia mawasiliano (Speech pathology), Tiba Kazi (Occupational therapy) na Tiba Viungo (Physiotherapy) na shahada ya kwanza ya Sayansi ya Saikolojia ya Kitabibu (Clinical Psychology) kuanza mwaka huu 2024.

#NTTUpdates