×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

UHALIFU WADHIBITIWA VISIWANI ,VIONGOZI WA VIJIJI WAONYWA

Na Mwandishi wetu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limeendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yote majini na nchi kavu kupitia doria na misako inayo endelea.

Kupitia misako hiyo iliyofanyika siku mbili tarehe 15 na 16 mwezi huu, zaidi ya watuhumiwa 30 wa makosa mbalimbali wamekamatwa katika visiwa vya Soswa, Chembaya, Chamagati na Nyamango katika Halmashauri ya Buchosa, wilaya ya Sengerema.

Akizungumza na wananchi wa Kisiwa cha Soswa Januari 16.2025 kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafugwa ameonya vikali baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika maeneo ya visiwani wakiwemo baadhi ya viongozi wa vijiji wanaoshindwa kutoa ushirikiano na kuwaficha wahalifu katika maeneo yao.

“Viongozi wa vijiji mnawajibu wa kusaidia kuundwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi ili kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoanza kuchipuka kwenye maeneo yenu na sio kuwaficha wahalifu” ameonya kamanda Mutafugwa

Kamanda Mutafungwa, amesema kuwa operesheni zinazoendelea visiwani zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani mpaka anapoongea na wananchi hao siku ya jana, watuhumiwa 28 wanaojihusisha na vitendo vya ukahaba, watuhumiwa wawili waliokutwa na kete 157 za bangi, na wengine 10 wa makosa ya kihalifu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika visiwa na maeneo yote ya mkoa wa Mwanza sambamba na kutoa elimu ya usalama katika makundi yote ili amani na usalama viendelee kutawala katika mkoa wetu bila kusahau kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa nchi yetu ni letu sote hivyo tushirikiane kuzuia uhalifu” alisisitiza kamanda Mutafugwa

Aidha, amewataka wahalifu wote wanaosakwa kujisalimisha mara moja kwa Jeshi la Polisi kabla hawajafikiwa na mkono wa dora.

Pia, Kamanda Mutafugwa amewahakikishia hali ya usalama kwa wakazi wote wa mkoa wa Mwanza huku akisisitiza kuwa operesheni hiyo endelevu ina lengo la kukomesha vitendo vya uhalifu.

#NTTUpdates