×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

UTEKELEZAJI WA MIRADI ZANZIBAR UNAHITAJI KUZINGATIA WAKATI-RAIS MWINYI

Na Mwandishi wetu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema miradi ya kimkakati inayoendeshwa Zanzibar inahitaji kuzingatia wakati katika utekelezaji wake ili kuleta tija kwa Taifa.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na Ujumbe wa watendaji kutoka Kituo cha Nishati cha Oman uliofika kuelezea hatua za miradi wanayoisimamia hapa Zanzibar ikiwemo miradi ya Maji, Nishati na ukarabati wa Mji Mkongwe ambao ni urithi wa dunia.

Rais Dk. Mwinyi ameuhakikishia ujumbe huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itawapa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha miradi hiyo aliyoielezea kuwa na umuhimu mkubwa kwa Uchumi wa Zanzibar, maendeleo na ustawi wa wananchi wake.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho, Abdallah Humaid Al Ma’amary alisema, moja ya maboresho ya Mji Mkongwe ni kuufanya kuwa mji wa kisasa (Smart City) bila kuharibu uhalisia wa mji huo na kuzingatia vigezo na miongozo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuwa ni urithi wa dunia na kielelezo muhimu cha historia ya Zanzibar.

#NTTUpdates