
New York, Marekani
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema matumizi sahihi ya teknolojia katika mifumo ya Mahakama yanaweza ni nyenzo muhimu ya kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana, hususan wale wanaokumbwa na ukatili wa kijinsia.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 17 Machi, 2026 alipofungua mkutano uliondaliwa na Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) uliofanyika pembezoni mwa mkutano wa 70 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York, Marekani.

Akizungumza mbele ya Waheshimiwa Majaji, wajumbe na wataalam kutoka mataifa mbalimbali, Dkt. Gwajima amesema, usawa mbele ya sheria haupatikani kwa kuweka tu misingi ya kikatiba au kutunga sheria, bali unahitaji mifumo ya haki inayofanya kazi kwa vitendo na inayoweza kufikiwa kwa urahisi na wananchi.
Katika mjadala huo, Dkt. Gwajima amekipongeza Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kuwasilisha mada kuhusu namna Mahakama ya Tanzania inavyokabiliana na vikwazo vinavyokwamisha haki za kijinsia kupitia matumizi ya mifumo ya kidijitali katika mahakama ambapo, hatua hiyo imeonesha uzoefu wa Tanzania katika katika kuleta mageuzi na mabadiliko ya kidijitali kwenye Utendaji wa mfumo wa Mahakama na kuimarisha upatikanaji wa haki za kijinsia.

Dkt. Gwajima amesema, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa haki yanapunguza changamoto mbalimbali ikiwemo umbali wa kufika mahakamani, ucheleweshaji wa mashauri, pamoja na kuimarisha usiri wa taarifa kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na kupunguza changamoto ya manusura kujieleza kila wakati kuhusu yaliyojiri jambo ambalo linapunguza athari za kisaikolojia kwani, taarifa hutunzwa vema na mifumo ya kidigitali kwa kumbukumbu na katika mazingira ya usiri mkubwa.
Ameongeza kuwa, hatua hiyo imeongeza uwezo wa kukusanya takwimu zinazotenganisha taarifa za wanawake na wanaume, jambo linalosaidia katika kupanga sera na mikakati bora ya kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wote.

“Natambua mchango wa majaji wanawake katika kuendeleza mageuzi ya mfumo wa haki, kwani uongozi wao umechangia kuleta mabadiliko yanayozingatia utu, uwajibikaji na mahitaji halisi ya jamii.” amesema Waziri Dkt. Gwajima
