Na Mwandishi wetu.
Waziri Kombo aongoza Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 9 Desemba 2024 kutokea Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ambao umewakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Nchi Wanachama wa SADC ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Malawi ni Mwenyekiti Ajaye na Zambia ni Mwenyekiti anayemaliza Muda Wake umejikita katika kujadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hususan bajeti ya Misheni ya kanda iliyopo nchini humo kwa kipindi cha kuanzia mwezi Desemba 2024 hadi Desemba 2025.
Wakati wa Mkutano huo Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa Nchi Wanachama kuendelea kuchangia Misheni hiyo kwa Wizara za Fedha kutoa kipaumbele kwa michango hiyo pamoja na kuoanisha juhudi za kijeshi na kidiplomasia.
Taarifa ya Kikao hicho itawasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kitakachofanyika tarehe 11 Desemba, 2024 na kuongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.
Kikao hicho kilichotanguliwa na Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo.
#NTTUpdates