Na Mwandishi wetu.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasili mjini St. George’s, nchini Grenada ambapo atamwakilisha Rais Daktari Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum – ACTIF 2025) unaotarajiwa kuanza Julai 28–30, 2025 katika kituo cha mikutano cha Radisson.
Mkutano unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa ya Afrika na visiwa vya Karibian.Waziri Mkuu anashiriki mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali, kukutana na viongozi wa mataifa mengine, pamoja na kushiriki katika mikutano ya uwili na wawekezaji wakubwa, ikiwa ni dhamira ya Tanzania ya kuendeleza juhudi zake za kuvutia wawekezaji wa kimataifa ili kusaidia katika kujenga uchumi wa kisasa na shindani duniani.
Ushiriki wake katika mkutano huo akimwakilisha ni mwendelezo wa dhamira ya dhati ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuifungua nchi kimataifa na kuimarisha ushirikiano, ili kuchochea maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.
Baadhi ya maeneo muhimu ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo ni kuanzishwa kwa eneo la Biashara huria kati ya Afrika na Karibiani, kuimarisha baraza la biashara la Afrika na Karibiani, kuchochea uchumi na ubunifu pamoja na Kukuza uhusiano wa usafiri wa anga na baharini kati ya Afrika na Karibiani.
Mkutano huo umeratibiwa na Jamhuri ya Granada pamoja na taasisi ya kifedha ya kimataifa yenye lengo la kukuza biashara ya bidhaa na huduma ndani na nje ya Afrika (Afreximbank).
#NTTupdates