Na Mwandishi wetu.
Watu watano wamefariki dunia papo hapo baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika Kijiji cha Bukumbi, Kata ya Idetemya, Tarafa ya Usagara, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Willbroad Mutafungwa, amesema ajali hiyo imetokea baada ya gari dogo aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba T 852 DGP, mali ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi, kulipita gari bila tahadhari na kugongana uso kwa uso na lori aina ya Sino Truck lenye namba T 541 DCH, mali ya Kampuni ya Nyanza.
Waliofariki ni Sr. Nelina Semeoni (60), raia wa Italia; Sr. Lilian Kapongo (55), mkazi wa Tabora; Sr. Damaris Matheka (51) na Sr. Stellamaris Kamene Muthin (48), wote raia wa Kenya; pamoja na dereva Boniphace Peter Msonola (53), mkazi wa Bukumbi.
Majeruhi pekee ni Sr. Pauline Vicent Mipata (20), Msimamizi wa wanafunzi wa shule hiyo, ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Miili ya marehemu imehifadhiwa Bugando kwa uchunguzi, huku dereva wa lori, Venance Manampo Mashaka (61), mkazi wa Buhongwa, akishikiliwa na Polisi kwa mahojiano.
#NTTupdates