×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

DIWANI ATOA KIWANJA KWAAJILI YA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI

Na Mwandishi wetu.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Waheshimiwa Madiwani nchini kuiga mfano wa Diwani wa Kata ya Kiutu Mhe. Malaki Malambo aliyetoa kiwanja chenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 6400 kwa ajili ya kujenga shule ya Sekondari Kiutu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

Mchengerwa ametoa wito huo kwa madiwani wote nchini, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua na kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

Mchengerwa amesema, kitendo cha Diwani wa Kata ya Kiutu Mhe. Malaki Malambo kutoa kiwanja chake ni ishara ya upendo wa dhati alionao kwa wananchi ambao walimchagua ili awaongoze na kuwaletea maendeleo.

“Ninawaomba Waheshimiwa Madiwani wengine kuiga mfano mzuri wa Mhe. Malambo alijejitoa kwa wananchi wake kwa kutoa kiwanja kilichowezesha ujenzi wa shule ya Sekondari Kiutu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Ili kuunga mkono kitendo cha Diwani Malambo kutoa kiwanja, Waziri Mchengerwa ameanisha kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI itafanya mchakato wa kuwezesha kukamilisha ujenzi wa jengo la Shule ya Kiutu ili shule hiyo mwakani ipokea wanafunzi 555 tofauti na mwaka huu ambapo imepokea wanafunzi 400.

Mchengerwa amesema majengo 8 yaliyokamilika hayawezi kuchukua wanafunzi zaidi ya 400, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kukamilisha majengo yaliyosalia ili wanafunzi wapate miundombinu bora na rafiki ya kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

“Nikihitimisha ziara yangu, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Ofisi ya Rais-TAMISEMI aje na timu yake kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika ili tuwasilishe ombi la fedha kwa Mhe. Rais na hatimaye tuweze kukamilisha ujenzi wa shule hiyo,” Mhe. Mchengerwa amehimiza.

Waziri Mchengerwa yupo mkoani Arusha kwa ajili ya ziara ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji kwa wasimasmizi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.

#NTTUpdates