Hali ya ulinzi na usalama ndani ya Ziwa Victoria imeimarika kutoka na tathmini zilizofanyika kupitia vikao vitano vilivyohusisha Maofisa wa Jeshi la Polisi, maafisa uvuvi pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na ulinzi wa rasilimali za Ziwa Victoria.
Akitoa taarifa hiyo Mkuu wa Usimamizi wa Vikosi Maalum vya Polisi kutoka Kamisheni ya Opereseheni na Mafunzo, Makao Makuu ya Polisi Dodoma (DCP), Ferdinand Mtui katika kikao maalum kilichohusisha makamanda wa Polisi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na wadau wa uvuvi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni za Jeshi la Polisi nchini, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mihayo Msikhela amesema katika kipindi cha mwaka 2019-2020 kuliibuka uhalifu ndani ya Ziwa Victoria ikiwemo mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, uporaji wa nyavu, samaki na boti za Injini.
SACP Mihayo amesema vitendo hivyo vilipelekea majeruhi na vifo kwa baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara ziwani lakini kwa sasa matukio hayo yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
“Tupo tayari kushirikiana na wadau wote wa uvuvi wa nchini dhidi ya uhalifu wowote wa ndani na nje ya mipaka yetu, wale ambao wanavua kwa makusudi huku wakijua kuwa wamevuka na wapo kwenye maeneo yetu wawe tayari kupambana na moto wa Jeshi letu na tukiwapata tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria,”ameeleza Msikhela.
Amesema sheria za nchi zimeweka bayana iwapo mtu akiingia nchini kinyume na utaratibu ikiwemo kukosa kibali cha kusafiria kuwa atakamatwa na kufikishwa mahakamani huku akiwasisitiza wavuvi wa Tanzania wasivuke mipaka ya Ziwa kwenda katika eneo la nchi jirani za Kenya na Uganda. Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akimwamilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla,ameeleza kuwa sekta ya uvuvi inachangia kwa asilimia 7 pato la Mkoa.
Amesema mkoa wa Mwanza umedhamiria kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano katika sekta ya uvuvi ya kuifanya Mwanza kuwa na uchumi wa bluu kwa kuanzisha miradi mbalimbali kupitia ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
“Ni sekta pekee ya uvuvi ambayo mtu anaweza kuwa na kiwango kidogo cha fedha na akafanikiwa hivyo samaki wasipokuwepo ziwani hata uchumi wa Mkoa unashuka,” amesema Makilagi Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Wilbrod Mutafungwa amesema wamekuwa wakitoa elimu ya uvuvi salama kupitia mikutano mbalimbali na Opereseheni zilizosaidia kupunguza uhalifu ndani ya ziwa Victoria.