Na Mwandishi wetu.
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini ( REA) kuongeza kasi ya ununuzi wa transforma zinazozalishwa na kiwanda cha Tanalec kwa kuwa Taasisi hizo ni wamiliki wa sehemu ya hisa za kiwanda hicho, ili kukiwezesha kuendelee kukua na kuongeza ajira nchini.
Dkt. Jafo ameyasema hayo Agosti 24, 2024, Mkoani Arusha, alipotembelea viwanda mbalimbali na kuongea na wafanyabiashara pamoja na Maafisa Biashara wa Mkoa huo, kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji lakini pia kusikiliza changamoto za wafanyabiashara, ili kupata njia bora ya kuzitatua kwa kushirikiana na Taasisi nyingine husika ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake kanda ya Kaskazini katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Aidha Dkt. Jafo amelielekeza Shirika la Taifa la Maendeleo NDC kuhakikisha linapata mwekezaji makini kwa ajili ya kiwanda cha matairi cha General Tyre East Africa ( GTEA) Limited ili kifufuliwe tena na kuanza uzalishaji wa matairi ambapo itasaidia kuongeza ajira kwa vijana na taifa kiujumla.
Waziri Jafo pia amewataka watanzania kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha sekta ya viwanda na biashara inasonga mbele kwa kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo miundombinu ya maji, barabara na umeme.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, ameahidi kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Fedha na TAMISEMI ili kuhakikisha changamoto zote za wafanyabiashara zinatatuliwa ili kuhakikisha viwanda vyote Mkoani humo vinafanya kazi.
#NTTupdates