Na Mwandishi wetu.
Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa taarifa ya mwenendo wa viashiria vya kiuchumi kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2024, ikionyesha ukuaji wa uchumi katika sekta za utalii, nishati, na mawasiliano.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 19, 2024 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, amesema idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kutoka milioni 1.2 mwaka 2023 hadi milioni 1.5 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 20.
Amesema Idadi ya watalii imeongezeka kwa zaidi ya mara mbili tangu mwaka 2021, kutoka watalii 624,396 hadi 1,560,641 mwaka huu na Ukuaji huu umetokana na juhudi za Serikali kutangaza vivutio vya utalii kupitia miradi kama filamu ya Royal Tour na Amazing Tanzania.
“Watalii wengi waliotembelea Tanzania walitoka Marekani (112,579), Ufaransa (79,079), Ujerumani (76,021), Italia (75,543), na Uingereza (67,180). Kutoka bara la Afrika, Kenya iliongoza kwa watalii (156,674), ikifuatiwa na Burundi (153,497), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (49,963), Zambia (46,599), na Rwanda (45,810).” Amesema Masolwa.
Akizungumza kuhusu ukuaji wa uchumi kwenye sekta ya Nishati Masolwa amebainisha kuwa Katika kipindi hicho, uzalishaji wa umeme uliongezeka kwa asilimia 11.8, kutoka saa za kilowati bilioni 7.6 mwaka 2023 hadi bilioni 8.5 mwaka 2024.
Masolwa ameeleza kuwa chanzo kikubwa cha uzalishaji wa umeme kilikuwa gesi (asilimia 51.8), maji (asilimia 46.9), na mafuta (asilimia 1.2).
“Kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kunatokana na uzinduzi wa mradi wa bwawa la Julius Nyerere, ambao umeongeza uzalishaji wa umeme kutoka maji na kupunguza utegemezi wa gesi asilia,” amesema.
Masolwa amebainisha kuwa Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2024, muda wa mawasiliano kupitia simu umeongezeka kutoka dakika bilioni 105.9 mwaka 2023 hadi bilioni 115.7 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 9.2 nakuongeza kuwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi.
“Huduma za mawasiliano ni kichocheo muhimu cha tija katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma. Ukuaji huu umechangia kuboresha maisha ya wananchi na uchumi kwa ujumla,” Amesema Masolwa.
#NTTupdates