
Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linamsaka dereva aliyesababisha ajali iliyopelekea kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine wawili katika mtaa wa Nyamadoke kata ya Nyamhongolo wilaya ya Ilemela
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Naibu kamishna Wilbrod Mutafungwa amesema ajali hiyo imetokea jana Machi 24, 2026 majira ya saa kumi na mbili na nusu jioni ambapo pikipiki ya magurudumu matatu ya kubeba mizigo [guta] yenye namba za usajili MC 433 DGU aina ya Wanhoo iliyokuwa ikiendeshwa na Zabron Simon iliyokuwa ikitokea Barabara ndogo na kuingia Barabara kuu iligongana uso kwa uso na gari lenye namba T 406 EGZ aina ya Howo Truck ambalo lilikuwa likitokea Buswelu kuelekea Nymhongolo na kupelekea dereva wa pikipiki kupoteza maisha hapo hapo
Aidha kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa baada ya kugongana uso kwa uso gari hilo lilipoteza uelekeo na kugonga banda la mgahawa lililokuwa upande wa kushoto wa Barabara ambapo walikuwepo wanawake wawili wanaofanya biashara ya chakula na kuwasababishia majeraha ambapo walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa huo wa Mwanza ya Sekou Toure kwa ajili ya kutibu majeraha waliyopata
Kamanda Mutafungwa amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi wa gari lenye namba T 406 EGZ lililokuwa likitokea Buswelu kuelekea Nyamhongolo ambapo dereva alikuwa akiendesha kwa kasi katika maeneo ya makazi ya watu bila kuchukua tahadhari lakini pia pikipiki ya magurudumu matatu iliingia katika Barabara kuu pasipo kuchukua tahadhari
Katika hatua nyingine kamanda Mutafungwa amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure kwa ajili ya uchunguzi zaidi huku juhudi za kumtafuta dereva aliyekimbia baada ya kusababisha ajali zikiendelea





NTTUPDATES.