Na Mwandishi wetu
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema licha ya changamoto mbalimbali na mtazamo hasi unaoelekezwa kwa TRA mara kwa mara, watumishi wake wameendelea kufanya kazi kwa weledi, kujituma, na kuzingatia maslahi ya Taifa.
Mwenda ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia katika ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa Tathmini ya Utendaji Kazi wa TRA, uliofanyika leo Julai 8, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
“Mafanikio ya TRA hayapatikani bila juhudi; kuna watu wanaojitolea usiku na mchana kufanya kazi hizi.
Wapo wengi sana lakini wanaoongoza ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Najua hatupendwi sana, na wala hatutarajii kupendwa sana.
Tunachotakiwa kufanya ni kufanya kazi sahihi licha ya maneno. Licha ya vyote, bado wafanyakazi wameendelea kuhakikisha wanasaidia biashara ziendelee na nchi inakusanya kinachotakiwa,” amesema Kamishna Mkuu huyo wa TRA.
Aidha, amegusia lengo jipya la TRA kk wa mwaka wa fedha 2025/2026 ni kukusanya kiasi cha shillingi Trillion 36 ambazo anaamini zinapatikana kwa kazi nzuri watakayoifanya kwa kushirikiana na waajiriwa wapya huku akituma salamu kwa viongozi wa TRA katika maeneo mbalimbali kuendeleza uhusiano mzuri na walipakodi kwa kuwa nao karibu zaidi.
#NTTupdates.