×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

MAGWIJI WA TIBA RADIOLOJIA DUNIANI WAKUTANA MUHIMBILI

Na Mwandishi wetu.

Magwiji wa tiba radiolojia duniani ambao hutumia vifaa kama vile CT-Scan, MRI, Xray, Angiography system, Utrasound n.k kufanya uchunguzi na kutibu magonjwa mbalimbali kupitia matundu madogo, mapema wiki hii wamekutana Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutathmini hali ya utoaji huduma hiyo nchini na kujadili mbinu za kuongeza wigo wa huduma hiyo kuanzia ngazi ya hospitali zote za rufaa za kanda, kwani kwa sasa inatolewa tu kupitia hospitali ya taifa, maalum na hospitali chache za kanda.

Tiba radiolojia ni aina ya taaluma ya matibabu ambapo daktari bingwa mbobezi wa tiba radiolojia hutumia teknolojia ya picha (CT, Xray, Ultrasound) kumuongoza kufanya uchunguzi au tiba kupitia matundu madogo mwilini bila kufanya upasuaji mkubwa ili kuzibua mishiba ya damu iliyoziba au kusinyaa, kupunguza ukubwa wa uvimbe au vivimbe, kutibu kuvuja kwa damu (kunakosababishwa na kupasuka kwa mishipa midogo ya kwenye tumbo na utumbo), kuingiza dawa ya kutibu uvimbe wa saratani moja kwa moja kupitia mishipa ya damu inayolisha uvimbe, kuchepusha damu kwenye ini lililonyafuka na matibabu mengine mengi.

Mratibu wa Tiba Radiolojia na Tiba Mtandao kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Grace Bash amesema lengo la Serikali ni kupunguza gharama za huduma hizo kutokana na uwekezaji ilioufanya kupitia vifaa tiba na kwa kutambua umuhimu huo, wizara ina kitengo maalum kinachoratibu upatikanaji wa huduma hizo nchini ambacho kwa sasa kipo katika hatua kadhaa za utengenezaji miongozo ya huduma hiyo.

#NTTupdates