×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

MAKULUBALIANO YA NMB NA JKCI KULETA AFUENI KWA WATOTO 13,800 WENYE MARADHI YA MOYO DAR

Na Mwandishi wetu.

BENKI ya NMB na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wamesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha benki hiyo kusaidia gharama za matibabu ya watoto wanaotibiwa katika taasisi hiyo kwa kiasi cha Sh. Bilioni 1 kwa miaka minne, sawa na Sh. Milioni 250 kwa mwaka.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, mbele ya wanasheria wa taasisi hizo.

Akizungumza wakati wa utilianaji Saini huo, Bi. Zaipuna alisema Sekta ya Afya ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa taasisi yake, ambayo inatambua na kuthamini juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo inachangia asilimia 70 ya matibabu ya watoto hao.

Alibainisha kuwa, kwa mujibu wa makubaliano waliyosaini, NMB inaenda kusaidia asilimia 30 ya gharama za matibabu, ambayo ni takribani Sh. Mil. 4 kwa mtoto mmoja, ambayo bado ni kubwa kwa wazazi na walezi wengi nchini kumudu kulipa na kuwezesha tiba kwa watoto wao.

“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, zaidi ya watoto 13,800 huzaliwa na changamoto za moyo kwa mwaka hapa Tanzania, wengi miongoni mwa wazazi wa watoto hao wanashindwa kumudu gharama za matibabu, na hivyo watoto wengi huchelewa kupata matibabu stahiki na hivyo afya zao kuwa mashakani.

Kabla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, aliishukuru NMB kwa kukubali kuingia makubaliano hayo, aliyoyataja kama yanayoenda kuunga mkono juhudi za Rais Dk, Samia Suluhu Hassan, aliyempongeza kwa kufanya mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya nchini hususani JKCI.

“Dk. Samia amefanya makubwa sana katika Sekta ya Afya na JKCI ni miongoni mwa mnufaika wa juhudi hizo, mapinduzi aliyoleta yanaifanya JKCI kuwa taasisi kubwa na ya kwanza Afrika linapokuja suala la tiba za maradhi ya moyo, oparesheni salama na uokozi wa vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo, ambavyo viko chini ya asilimia 5.

Alibainisha ya kwamba Historia ya JKCI haiwezi kuelezewa popote bila kuitaja NMB, ambayo imefanya makubwa hapo tangu 2015, ambako imesaidia sio tu wagonjwa wanaotibiwa hapo, bali hata wafanyakazi wa taasisi kwa kuwapa huduma bora na rafiki, ikiwemo mikopo nafuu inayowaongezea ufanisi kazini.

“Kuthibitisha kuwa huu ni muendelezo, mwaka 2017 NMB ilijenga eneo la mapunziko ya wagonmjwa wa nje chini ya uongozi wa Profesa Mohamed Janabi, lakini mwaka 2022 wafanyakazi wa NMB walichanga sehemu ya mishahara yao kusaidia gharama za matibabu ya watto waliofanyiwa opearesheni hapa.

Dk. Kisenge aliahidi kwamba JKCI itazingatia makubaliano yaliyosainiwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu juu ya maradhi ya moyo, na kwamba wataendelea walipoishia kwa sababu tayari taasisi yake imeshazunguka katika mikoa 17 na kuonana na kusaidia wagonjwa zaidi ya 17,000.

#NTTupdates