×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

MASELELE AHUKUMIWA JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA MJUKUU WAKE

Na Mwandishi wetu.

Mahakama ya Wilaya Sengerema, mkoani Mwanza, imemuhukumu Lucas Maselele (56), mkazi wa kijiji cha Lugata kwenda jela miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mjukuu wake (13) (jina linahifadhiwa) kwa sababu za kisheria.

Hukumu hiyo imesomwa leo Machi 13,2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka Katika kesi hiyo ya Jinai namba 16492/2024 .

Awali, Mwendesha Mashtaka wakili wa Serikali Nyamhanga Tissoro aliieleza Mahakama kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 04, 2024, katika Kijiji cha Lugata, wilaya ya Sengerema kwa kumbaka mjukuu wake wakati mke wake ameenda msibani mpaka alipofumaniwa na mke wake akifanya kitendo hicho kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) pamoja na kifungu cha 131(1) vya sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya Kwanza tarehe 14.06.2024 baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi na kusomewa shtaka hilo ambapo alikana kutenda kosa hilo.

Upande wa Jamhuri ulileta ushahidi na shauri lilianza kusikilizwa katika mahakama hiyo hadi leo Machi 13 ambapo mshtakiwa alijitetea na kuomba mahakama imuachie huru akidai ni njama tu zilizotengenezwa na mke wake.

Hata hivyo mahakama baada ya kupitia vifungu vya sheria sambamba na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ikiwemo ripoti ya mganga aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri wameweza kuthibitisha shtaka hilo bila ya kuacha shaka lolote kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo la kumbaka mjukuu wake.

#NTTUpdates