×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

MFAHAMU ANDERSON LUIS DE SOUZA (DECO) MCHEZAJI WA KWANZA KUPEWA TUZO YA FIFA YA KIUNGO BORA WA MWAKA

Makala Maalum.

Anderson Luis de Souza maarufu kama Deco miongoni mwa viungo bora waliowahi kubeba tuzo ya FIFA ya kiungo bora wa mwaka.

Anderson Luís de Souza alizaliwa Sao Bernardo de Campo 27 Agosti 1977, nchini Brazili na baadae kuomba uraia wa Ureno na kukubaliwa.

Deco pia yupo kwenye rekodi ya wachezaji wachache duniani waliowahi kushinda taji la klabu bingwa la Ulaya mara mbili akiwa klabu mbili tofauti, mwaka 2004 akiwa na Porto na mwaka 2006 akiwa na FC Barcelona.

Deco alianza kusakata kabumbu kwenye timu ya vijana ya Nacional mwaka 1995 mpaka 1996, baadae alienda kujiunga na Corinthians na kucheza kwa msimu mmoja tu, akicheza michezo 2 na kufunga goli moja.

Mwaka 1997 alijiunga na CSA lakini haukuwa msimu mzuri Kwani hakupata nafasi ya kucheza. Mwaka 1998 alijiunga na Benfica ambapo pia alikosa nafasi ya kucheza na klabu hiyo ikaamua kumpeleka kwa mkopo klabu ya shambani ya Alverca na hapo ndipo mwamba huyo alianza kujipata baada ya kucheza michezo 32 na kufunga magoli 20.

Msimu mmoja baadae Deco alienda kujiunga na klabu ya Salgueiros. Akiwa Salgueiros, Deco aliandamwa na majeraha na akacheza mechi chache tu, hadi Porto ilipomnunua mnamo Machi 1999.

Akiwa na FC Porto msimu wake wa kwanza alifanikiwa kushinda taji la ligi kuu na kufanya kocha wake Antonio Simoes kumuona Deco kama mrithi wa Riu Costa ambaye alikuwa ni gwiji wa klabu hiyo na alifunga goli ndani ya sekunde ya 30 tu katika ushindi wa 1- 0 ugenini dhidi ya Molde katika Ligi ya Mabingwa ya Ulaya msimu wa 1999-2000.

Chini ya meneja José Mourinho msimu wa 2002-03, Deco alifunga mabao 10 katika mechi 30, alipewa kadi 17 za njano na kadi nyekundu moja.

Alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika fainali ya Ulaya ambapo Porto alishinda 3-2 dhidi ya Celtic.

Katika msimu wa 2003-04, Deco aliisaidia Porto kutwaa tena taji la taifa na kuiongoza timu hiyo kufika Fainali ya Klabu bingwa Ulaya mwaka 2004, ambapo Porto ilishinda 3-0 dhidi ya Monaco ya Ufaransa huku Deco akifunga bao la pili la katika mchezo huo.

Deco alishinda Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Klabu ya Ulaya pamoja na tuzo ya kiungo bora wa mashindano msimu huo pia.

Mwaka 2004 alijiunga rasmi na Barcelona ambapo alisaini mkataba huo baada ya kuisha mechi ya fainali dhidi ya inter Milan, kwa dau la Euro Milioni 15.

Akiwa huko alipata mafanikio mengi ikiwemo alitunukiwa tuzo ya Mpira wa dhahabu wa kombe la Dunia la klabu ya FIFA, tuzo ya mwanasoka bora na mchezaji bora wa mechi ya fainali licha ya kupoteza mbele ya inter Milan.

Mnamo Mei 14, 2005, Deco alicheza kwenye sare dhidi ya Levante, ambayo iliipa Barcelona ubingwa wa 17 wa La Liga. Deco alitajwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa Barcelona katika msimu wa 2005-2006.

Kwenye mchezo wa fainali wa Supercup ya Hispania Deco alifunga mara mbili na kuisadia Barcelona kubeba kombe hilo, akiwa Barcelona alicheza michezo 113 na kufunga magoli 31.

Tarehe 30 Juni 2008, Chelsea ilimsajili Deco kutoka Barcelona kwa kandarasi ya miaka mitatu kwa Euro milioni 10.

Ulikuwa usajili wa kwanza wa kocha mpya wa Chelsea Luiz Felipe Scolari, ambaye zamani alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ureno na alikuwa akimfahamu.

Deco alifunga mechi yake ya kwanza Chelsea kwenye Premier League kwa bao la umbali wa yadi 30 katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Portsmouth. Deco alfunga bao katika mchezo wake wa pili kwa Chelsea, mkwaju wa faulo wa kujipinda dhidi ya Wigan Athletic.

Uchezaji huu ulimpelekea kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu kwa mwezi AgostiDeco alicheza mechi yake ya kwanza ya UEFA Champions League akiwa na Chelsea tarehe 16 Septemba.

Deco alijeruhiwa wakati wa mazoezi, lakini alirejea kutoka kwa jeraha la paja mnamo Oktoba 19 na akaingia kama mbadala dhidi ya Middlesbrough.

Alitolewa kwa kadi nyekundu kwenye kichapo cha 3-1 na Roma mnamo 4 Novemba 2008. Kisha akafunga kiki ya baiskeli dhidi ya Bolton Wanderers mnamo tarehe 6 Desemba.

Kila Nabii na zama zake hatimaye Deco alipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza msimu wa 2008-09, kutokana matokeo mabaya ya Chelsea lakini pia, kufukuzwa kwa Kocha Scolari nayo ilichangia kuwa tatizo kwake kwenye klabu hiyo.

Moja ya mahojiano yake ambayo aliyefanya alinukuliwa akisema, “Sitaki kubaki Chelsea na sijapenda uzoefu wangu Chelsea.

” Kauli hizi zilikuja baada ya a Inter Milan, iliyokuwa inafundishwa na meneja wa zamani wa Chelsea, wakati huo José Mourinho, ilikuwa imepanga kumsajili nyota huyo, lakini ilishindikana baada ya Rais wa wakati huo wa Inter Milan Massimo Moratti alikataa kwa kigezo cha umri mkubwa wa nyota huyo.

Mwaka 2010 Deco alijiunga na Fluminense ya Brazili kwa mkataba wa miaka miwili akiwa mchezaji huru, akiwa huko alitwaa kombe la ligi mwaka 2010 na 2012.

Akiwa Fluminense akicheza michezo 56 na kufunga magoli 9.Mnamo tarehe 26 Agosti 2013, Deco alitangaza rasmi kustaafu, na kumaliza kazi yake ya miaka 17 kwenye soka la ushindani na kwa sasa gwiji huyo ni mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Barcelona.

#NTTupdates