Na Mwandishi wetu.
Mgombea urais kupitia Chama cha Kijamii (CCK), Bw. David Mwaijojele, ameambatana na mgombea mwenza wake Bw. Masoud Ally Abdallah kufika katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kuchukua fomu za kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza maara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo na Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, jijini Dodoma, Bw. Mwaijolole ameeleza kuwa endapo wananchi watakipa ridhaa chama chake kuongoza serikali, wataelekeza nguvu zao katika kushughulikia changamoto za ajira, kilimo, afya, pamoja na maslahi ya wastaafu.
“Tumeona mara nyingi watu waliopo kazini wanaogopa kustaafu kwa sababu ya mazingira yasiyoridhisha. Sisi CCK tuna mikakati mizuri ya kuwaandalia mazingira bora ya kustaafu ili vijana wapate nafasi hizo za ajira,” amesema Mwaijojele.
Aidha, ameongeza kuwa serikali ya CCK ikiingia madarakani, itaweka mkazo katika uboreshaji wa makazi ya watumishi wa umma kwa kuhakikisha wanajengewa nyumba ili waweze kuwa na maisha bora baada ya kustaafu.
Katika hatua nyingine, Mwaijojele aliahidi kuwa serikali ya chama chake itaweka utaratibu wa kuwakopesha waandishi wa habari kwa mfumo wa kuchangia kiasi kidogo kidogo cha fedha, ambazo zitarudishwa kwao mwishoni mwa mwaka ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Tutaanzisha mfuko wa kuwawezesha waandishi wa habari. Hata kama ni shilingi mia mia kwa mwezi, mwisho wa mwaka tutawarudishia fedha hizo kwa ajili ya maendeleo yao. Ilani ya CCK ni bora na ya kweli zaidi hata kuliko ya CCM,” amesisitiza.
Chama cha CCK ni miongoni mwa vyama vinavyowania nafasi ya kuunda serikali, kikijitangaza kwa sera zake zinazolenga kuboresha maisha ya Watanzania kwa njia ya maendeleo shirikishi na jumuishi.
#NTTupdates