Na Mwandishi wetu.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandiai Chagu Ng’oma amemtaka Mkandarasi M/S Dimetoclasa Real Hope Limited anayejenga mradi wa Hospitali ya Rufaa yenye hadhi ya Mkoa Wilayani Ukerewe kuzingatia muda na ubora wa kazi ili thamani ya fedha zilizowekezwa ionekane.
Ametoa agizo hilo leo jumamosi tarehe 11 Januari, 2025 wakati wa kikao cha ukaguzi wa utekelezaji wa mradi huo kilichofanyika kwenye eneo la ujenzi huo katika kijiji cha Bukindo Nansio wilayani Ukerewe.
Mhandisi Chagu amesema, serikali imetenga fedha zaidi ya Tshs. Bilioni 25 ili wananchi walio katika Kisiwa hicho waweze kupata huduma za kibingwa bila kusafiri kwenda Mkoani Mwanza ambako ni mbali zaidi na kwa kutumia usafiri wa maji.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana matumaini makubwa sana na Mkandarasi ambaye atatekeleza mradi huu na wengine wote wanaosimamia sasa naomba kila mmoja atimize wajibu wake ili kukamilisha kwa wakati mradi huo.” Amesisitiza Mhandisi.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba ametoa wito kwa mkandarasi na mshauri elekezi kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa karibu na kuwasilisha taarifa kila wapatapo changamoto ili kuzimaliza kwa pamoja na kuufanya mradi ufanikiwe na kuweza kufikia lengo la serikali la kuwapatia wananchi huduma bora na za afya na za kibingwa.
Wakala wa Usimamizi wa Ujenzi huo kutoka M/S Dimetoclasa Realhope Limited, Mhandisi John Bhoke ameahidi kujenga hospitali hiyo kwa kasi na kwamba atakidhi matakwa ya Mkataba (muda na ubora) kama sera ya kampuni hiyo inavyodhihiri.
Mkandarasi wa ujenzi wa hospitali hiyo alikabidhiwa rasmi kazi tarehe 27 desemba, 2024 ambapo mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 hadi kufikia Juni 30, 2026 na tayari serikali ilishatoa Tshs. Bilioni 6 kwa awamu ya kwanza.
#NTTUpdates