Na Mwandishi wetu.
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi katika mkakati wake wa kuboresha sekta ya Uvuvi na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ipo mbioni kuanza doria ziwa Victoria, kwa kutumia ndege zisizo na rubani lengo likiwa ni kuboresha sekta hiyo na kuchangia zaidi katika pato la Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo katika mkutano wa kupokea maoni ya kuboresha kanuni za uvuvi na wadau wa sekta hiyo kwenye ukumbi wa mikutano wa Nyakahoja, Mkurugenzi wa uvuvi Prof. Mohamed Sheikh amebainisha Serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wa bluu utakao kuwa na tija kwa mwananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tunaanzia na ndege 5 na ziwa Victoria tutakuwa nazo mbili na hili zoezi litaanza mwaka ujao wa fedha,hatua hii itasaidia kutokomeza uvuvi haramu na kuwa na uhakika wa usalama wa viumbe maji,”amesisitiza mkurugenzi wa uvuvi wakati wa kufungua kikao kazi hicho cha kupokea maoni.
Ameongeza kuwa sekta ya uvuvi bado inachangia %1.8 katika pato la Taifa kiwango ambacho ni kidogo kulinganisha na ukubwa wa uchumi utakanao na sekta hiyo,hivyo mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha maboresho yenye tija yanafanyika.
Prof.Sheikh amekwenda mbali zaidi kwa kubainisha maboresho hayo sasa yatakuwa na mvuto zaidi kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi hasa baada ya kuwa na uhakika wa mazingira mazuri na wingi wa rasilimali zilizopo.
“Tumekuwa na utaratibu wa kuyafunga maziwa kwa muda hasa katika shughuli za uvuvi wa dagaa,tumeona namna zoezi hili lilivyokuwa na tija wanaporudi kuvua upatikanaji unakuwa wa kiwango kikubwa na soko linakuwa zuri”,mkurugenzi wa uvuvi.
Kwa upande wao wadau wa sekta ya uvuvi mkoani Mwanza wakiwemo wasindikaji wameishukuru Serikali kwa uboreshaji wa sekta hiyo na kuweka mazingira mazuri ya uvuaji wa kisasa zikiwemo boti zenye kuonesha dagaa au samaki walipo na ufugaji kwa kutumia vizimba.
“Ombi letu kwa Serikali tunaomba kupunguzwa kwa utitiri wa tozo ambao unapunguza vipato vyetu na kuiboresha mialo ambayo mingi haina mazingira rafiki hasa kwa wanawake wanaolazimika kuingia majini”Fatma Katula Msindikaji wa minofu ya samaki.
#NTTUpdates