×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

RAIS MWINYI:WAKUU WA MIKOA SIMAMIENI IPASAVYO SHERIA NA MIONGOZO YA ARDHI

Na Mwandishi wetu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia ipasavyo Sheria na Miongozo ya Ardhi ili kuepusha ujenzi holela unaoigharimu Serikali kulipa fedha nyingi za fidia kwa watu wasiostahiki.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi na Makaazi, hafla iliyofanyika katika Hoteli ya New Amani Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi leo tarehe 24 Juni 2025.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali italipa fidia kwa watu wenye hati na vibali halali vinavyostahiki, na si kwa wavamizi wa maeneo ya hifadhi ya barabara, maeneo ya wazi, na ekari za Serikali.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali italipa fidia kwa watu waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora za makaazi, na kuzitaka taasisi husika kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Maadhimisho hayo yalienda sambamba na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kondominio, uzinduzi wa Muongozo wa Tathmini na kukabidhi mipango ya kina ya matumizi ya ardhi kwa Wakuu wa Mikoa.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kwa ubunifu wa kuanzisha Wiki ya Ardhi na Makazi, na kutoa rai ya kuendelezwa kwa maadhimisho hayo kufanyika kila mwaka.

#NTTUpdates