×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

RAIS SAMIA MGENI RASMI GRAND BUNGE BONANZA

Na Mwandishi wetu.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha kubwa la michezo na burudani la CRDB – Grand Bunge Bonanza, litakalofanyika Jumamosi, Juni 21, 2025, katika viwanja vya Sekondari ya John Merlini, Miyuji jijini Dodoma.

Bonanza hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Bunge na Benki ya CRDB – ambaye ni mdhamini mkuu – linabeba kaulimbiu isemayo “SHIRIKI UCHAGUZI MKUU, KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU” na linatarajiwa kuwa la aina yake likiwakutanisha wabunge, watumishi wa Bunge na taasisi mbalimbali za Serikali kwenye michezo ya ushindani na burudani.

Mwenyekiti wa Bonanza hilo, Mhe. Festo Sanga amesema michezo itakayopambwa ni pamoja na mpira wa miguu, pete, kikapu, kuvuta kamba, mpira wa wavu, pamoja na michezo ya jadi na burudani kama taarabu, dansi, ngoma za asili, ushairi na vichekesho.

Mbali na kushuhudia mitanange ya kusisimua, wananchi wa Dodoma wamealikwa kushiriki katika shamrashamra hizo zitakazoanza saa 1:00 asubuhi, huku zawadi mbalimbali, medali, tracksuit, jezi na kifungua kinywa zikitolewa kwa washiriki wote.

Benki ya CRDB ambayo ni mdhamini mkuu wa bonanza hilo, imetoa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 130.

Mwakilishi wa benki hiyo, Ntully Mwambapa, alisema kuwa CRDB itaendelea kushirikiana na Bunge kuandaa matukio ya kijamii na kimaendeleo yanayolenga afya, mshikamano na ustawi wa wananchi.

“Tunatambua nafasi ya michezo katika kuleta watu pamoja, Bonanza hili pia ni sehemu ya kuwapongeza wabunge kwa utumishi wao wa miaka mitano,Tunatoa wito kwa wananchi wote wa Dodoma kushiriki,” alisema Ntully.

#NTTupdates