Na Mwandishi wetu.
Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, akiambatana na mgombea mwenza wake Devotha Minja, amechukua rasmi fomu za kuwania nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Akizungumza jijini Dodoma leo Agosti 12 ,2025 mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, Mwalimu alieleza kuwa yeye pamoja na mgombea mwenza wake wanaingia katika kinyang’anyiro hicho wakiwa huru na wasafi, bila mizigo ya kisiasa, kiuchumi au kihistoria.
Alisisitiza kuwa dhamira yao ni kuleta mabadiliko ya kweli yanayolenga kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kulinda maslahi ya wananchi.
“Tunatamani kuona Bunge lenye uhuru, Mahakama inayofanya kazi kwa uhuru, Serikali inayosikiliza na kutekeleza matakwa ya wananchi badala ya kulindana, pamoja na vyombo vya habari vyenye uhuru wa kuhabarisha bila woga.
Tunataka kuona wananchi wenye furaha na siyo hofu,” amesema Mwalimu.Aidha, amesisitiza kuwa wao kama wagombea hawana hofu yoyote kuhusu upya wao katika siasa au nafasi wanayoitaka, kwani wanayo rekodi nzuri ya utendaji, maono ya dhati, na hawabebeshwi mizigo ya ahadi au deni kwa mtu yeyote.
“Historia zetu na utendaji kazi wetu unatuweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa Rais na Makamu wa Rais huru wa kufanya maamuzi kwa maslahi ya Watanzania wote. Hatuna deni kwa mtu yeyote, hivyo tupo huru kulitumikia taifa bila kikwazo,” ameongeza.
Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, ambapo vyama mbalimbali vinaendelea kuwasilisha majina ya wagombea wao kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
CHAUMMA ni miongoni mwa vyama vinavyopigania mageuzi ya kisiasa na kijamii nchini, kikilenga kujenga Tanzania yenye usawa, haki na maendeleo kwa wote.
#NTTupdates