Na Mwandishi wetu.
Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Sekta ya Nishati ni moja kati ya Sekta tatu nchini ambazo zimechangia ukuaji wa pato la Taifa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2025.
Kapinga ameyasema hayo wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji Bungeni Jijini Dodoma.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ukiangalia kwa tathmini kati ya mwaka 2024 hadi 2025 Sekta ya Nishati imefanya vizuri katika kuchangia pato la Taifa, Sekta hii imetoka asilimia 5.8 mwaka 2015 na sasa hivi tunazungumzia asilimia 14.4”. Amesema Mhe. Kapinga
Ameongeza kuwa, Sekta ya Nishati imeweza kufanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika miradi ambapo amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa.
“Katika Gesi na Mafuta yamepatikana mafanikio makubwa sana ikiwemo uendelezaji wa miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia, katika kitalu cha Mnazibay na Songosongo Serikali imeweza kuzalisha futi za ujazo bilioni 25.51 kwa kipindi cha miaka minne kwa kila kimoja.
Ameongeza kuwa, Serikali imesaini mkataba katika kitalu cha Ruvuma Ntorya na sasa hivi kipo katika hatua za awali katika kuzalisha na kuendeleza gesi asilia.
Amesema katika kipindi cha miaka minne Sekta ya Nishati imepata mafanikio makubwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ambapo Serikali imeweza kuongeza hisa katika kitalu cha MnaziBay kutoka asilimia 20 hadi kufikia asilimia 40.
#NTTupdates