Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Waso hadi Loliondo yenye urefu wa kilomita 10 iliyopo katika Wilaya ya Ngorongoro kufanya kazi kwa weledi ndani ya muda aliyopewa ili wananchi wa maeneo hayo waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi bila kuwa na kikwazo cha miundombinu ya barabara.
Makonda amebainisha hayo leo wakati wa utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami inayokwenda kujengwa kutoka Waso hadi Loliondo Wilaya ya Ngorongoro.
“Barabara hii imesubiriwa kwa muda mrefu sana. Sasa kazi imeanza rasmi, nimtake mkandarasi anayetekeleza mradi huu awe na kasi sana kwa kufanya kazi mchana na usiku ndani ya miezi 12 aliyopatiwa”, amesema Makonda.
Sambamba na hilo, Makonda amesema kuwa kutokana na mkoa wa Arusha kuwa kitovu cha shughuli za utalii nchini ujenzi wa miradi hii ya barabara inaendelea kufungua fursa zaidi kwa wananchi na kwasasa zaidi ya Tsh. Billion 11 zinakwenda kutumika kwaajili ya kutekeleza miradi ya barabara na madaraja katika Halmashauri za Arusha DC, Meru na Longido.
Makonda amesema ujenzi wa barabara ya Waso hadi Loliondo ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha miundombinu inazidi kufika hadi maeneo ya pembezoni mwa nchi ili kuendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi ndani ya Taifa.
#NTTupdates.