×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

SERIKALI YATOA MAELEKEZO KWA WAOMBAJI AJIRA KUJIUNGA NA MIFUMO YA TEHAMA

Na Mwandishi wetu.

SERIKALI imewataka waombaji wa ajira Serikalini kujiunga na mifumo ya Tehama ya Serikali, ikiwemo Mifumo wa Ajira Portal.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 11,2025 jijini Dodoma ambapo amesema hatua hiyo ni muhimu ili waombaji wapate taarifa sahihi na za haraka kuhusu nafasi za kazi zinazotangazwa na serikali.

Simbachawene amehimiza kuwa kujiunga na mifumo hiyo kutawasaidia waombaji kujisajili na kufuatilia maendeleo ya maombi yao kwa urahisi.

Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa uwazi na ufanisi katika mchakato wa ajira, akisema ni lazima waombaji wafuate miongozo na kutumia teknolojia ili kuongeza nafasi zao za kupata kazi.

Amekumbusha kwamba serikali inafanya juhudi kubwa za kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza nafasi za ajira.

Aidha, amewataka vijana kujiandaa vizuri kwa ajili ya soko la ajira kupitia mafunzo na ujuzi wa kisasa, huku akiwashauri waombaji kuwa na subira katika kutafuta ajira, kwani serikali ina nia ya kutoa fursa zaidi kwa wananchi.

Waziri Simbachawene amefafanua kuwa Sekretarieti ya Ajira inatekeleza mchakato wa kuajiriwa kwa njia ya kidigitali kupitia “Ajira Portal”, ambapo waombaji wanatuma maombi yao mtandaoni na kupata mrejesho wa papo hapo na Mchakato huu unajumuisha hatua tatu ambazo ni usaili wa kuandika, usaili wa vitendo, na usaili wa mahojiano.

Aidha, ametangaza kuwa kuanzia Januari 14 hadi Februari 24, 2025, usaili wa kada za Ualimu utafanyika nchini, ukilenga kujaza nafasi 14,648 ambapo Usaili huo utahusisha waombaji kufanya mtihani katika mikoa yao, hivyo kupunguza gharama za usafiri.

” Waombaji wanatakiwa kuhuisha taarifa zao katika Ajira Portal na kubeba vyeti vyao halisi siku ya usaili” Amesema

#NTTupdates