Na Mwandishi wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi .Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakaribia kumaliza ujenzi wa madarasa 5,000 kuondoa zamu mbili kwa wanafunzi nchi nzima na kubakisha zamu moja.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipofungua rasmi Skuli mpya ya Sekondari Tumekuja iliopo Mwembeladu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe: 09 Januari 2024 katika shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vilevile Skuli hiyo mpya ya Tumekuja ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,755 kwa wastani wa uwiano wa wanafunzi 45 kwa darasa moja, tayari wanafunzi wameshapangwa wiki ijayo kuanza masomo.
Rais Dkt.Mwinyi amempongeza mkandarasi wa kampuni ya CRJE kwa kujenga Skuli ya kisasa ambayo ina maabara tatu ya kisasa, chumba cha kompyuta, maktaba na ukumbi wa mikutano.
Aidha Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itaendelea kujenga maghorofa katika sekta ya elimu kwa wanafunzi kutozidi 45 kwa darasa moja .
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kufanya uamuzi sahihi kwa faida ya nchi na kuyakarabati majengo ya mji mkongwe kwani ni urithi wa nchi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.