Na Mwandishi wetu.
Watumishi wa Serikali na mashirika binafsi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara wamepata mafunzo maalum ya kuongeza uelewa na kutafuta namna bora dhidi ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, yanayotolewa na One Stop Center kuanzia leo, tarehe 13 Oktoba 2025.
Mafunzo hayo yanayotarajiwa kukamilika tarehe 17 Oktoba 2025, yamelenga kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu njia bora za kupambana na vitendo vya ukatili katika jamii, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali katika utoaji wa huduma kwa waathirika.
Akifungua mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Dkt. Shadrack Makonda, amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kama chachu ya kuimarisha huduma za pamoja kwa waathirika wa ukatili, akibainisha kuwa uwepo wa huduma za afya, ustawi wa jamii na dawati la jinsia chini ya jengo moja umesaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa waathirika.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Maafisa Ustawi wa Jamii, Watumishi wa Afya, Jeshi la Polisi, Wanasheria pamoja na wageni kutoka nje ya nchi, wote wakiwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu namna bora ya kupambana na ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
Kwa upande wake, Daudi Donald, ambaye ni mwendeshaji wa mafunzo hayo, amesema kuwa Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa yenye changamoto kubwa za ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ambapo amewataka washiriki wote kutumia elimu waliyoipata kufikisha ujumbe kwa jamii na kuchukua hatua stahiki za kupunguza tatizo hilo.