×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

TANZANIA BADO TUNA FURSA NYINGI ZA UTALII – MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema bado kuna fursa nyingi hapa nchini ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje.

Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Agosti 21, 2024) wakati akizungumza na mamia ya wadau na washiriki waliohudhuria tukio la USIKU WA UTALII ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Tamasha la Kizimkazi 2024 lililofanyika kwenye uwanja wa Maendeleo ya Sheria wa Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar.

Amesema kwa kutumia fursa za utamaduni, wanyama na utalii wa fukwe Tanzania inaweza kuongeza idadi ya watalii kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na hali ilivyo sasa. “Hapa Kizimkazi tuna samaki aina ya pomboo ambaye ana sifa zote za kuingia kwenye utalii. Tuendelee kuimarisha utalii wa fukwe na tuwatumie pomboo kuchochea utalii kama ambavyo wenzetu wa Cuba wanawatumia.”

“Cuba ni nchi ndogo lakini inapokea watalii wengi sana. Wanao walimu wa kuwafundisha samaki hawa kucheza na binadamu, wanafundishwa kucheza muziki. Na sisi Tanznaia tunao pomboo wa kutosha. Ni kwa nini na sisi tusiige kutoka kwa wenzetu? Tufanye hili ili tuweze kuongeza fursa za utalii.”

“Bado tunazo fursa nyingi zaidi ya hizi, lakini hatujamudu kusheneneza soko letu kwa kutumia utalii wa ndani. Na sisi tunadhani utalii ni watu wa nje tu, hapana. Lakini utalii wa ndani ni eneo jingine linaloweza kuongeza idadi ya watalii nchini,” amesema.

Ili kuendelea kulikuza tamasha hilo, Waziri Mkuu amewataka Makatibu Wakuu wa wizara zinazohusika na masuala ya utamaduni kwa pande zote mbili wahakikishe wanaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni muasisi wa tamasha hilo pamoja na Kamati ya maandalizi ili idadi ya washiriki na wageni kutoka nje iweze kuongezeka.

“Matangazo na promosheni vianze miezi sita kabla ya tamasha ili watu waandae bajeti zao mapema na kwa njia hiyo tutaongeza hamasa ya ushiriki wa tamasha hili. Wizara na taasisi husika tumieni mitandao ya kijamii, tovuti, na vyombo vya habari ili kuongeza hamasa.”

Mapema, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga alisema waliandaa usiku huo maalum wa SIKU YA UTALII kama sehemu ya Tamasha la Kizimkazi 2024 ili kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vilivyopo Zanzibar.

“Tumeona ni vema tutumie fursa hii kutangaza vivutio vyetu kwani tunaamini tukitumia fursa hii, wageni wengi watakuja Zanzibar.”

Ametumia fursa hiyo kuwaomba watalii na wawekezaji wanaokwenda Zanzibar wazingatie suala la kuhifadhi na kutunza mazingira.

Naye, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Hamis Mwinjuma alisisitiza haja ya kuendelea kutumia utamaduni kama moja ya vichocheo vya utalii. “Tunapofanya matamasha haya ni lazima tulinde mila na desturi zetu,” alisema.